Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari MAELEZO

Serikali Yaunga Mkono Juhudi za UPTC

Dec 06, 2022

Na Georgina Misama – MAELEZO

Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na Umoja wa Wanahabari Tanzania (UPTC), wakati akitoa hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa umoja huo uliofanyika leo Jijini Dar es salaam.

Msigwa alisema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa waandishi wa habari kufanya kazi ikiwemo maboresho ya sheria mbalimbali zisizo rafiki kama vile Sheria ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016, ambapo mchakato wa mabadiliko hayo unaendelea.

“Serikali haipuuzi kazi nzuri inayofanywa na waandishi wa habari, endeleeni kuibua changamoto zilizopo katika jamii ili zipatiwe ufumbuzi, nawapongeza UPTC kupitia klabu za waandishi wa habari mikoani kwa kuhakikisha waandishi wanafanya kazi kwa weledi na uwajibikaji na kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi, nawahakikishia Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na ninyi,” alisema Msigwa.

Aidha, Msigwa aliwataka Waandishi wa Habari kuandika kwa kufuata misingi ya taaluma na kufanya kazi kwa kuzingatia miiko, utamaduni na maadili ya uandishi wa habari na kusisitiza kwamba Serika inawahakikishia usalama na uhuru katika kutimiza majukumu yao.

Msigwa aliwahamasisha Wadau wa Maendeleo, viongozi na Mamlaka mbalimbali za Serikali kuwawezesha waandishi wa habari katika kukabiliana na changamoto zao ikiwemo kuwapatia fursa za kutoka nje ya nchi ili kubadilishana uzoefu na waandishi wenzao pamoja na kufadhili habari za uchunguzi.

“Natoa wito kwa wadau mbalimbali wa habari wakiwemo viongozi wa mikoa na wilaya, hakuna ubaya mkoa au wilaya kuchangia fedha, vifaa au mafunzo kwa waandishi wa habari katika mkoa wako ili kuwawezesha Waandishi wa Habari kufanya kazi zao kwa ufanisi na kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Msigwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Lugha
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi