Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yatoa Kipaumbele Maslahi ya Wafanyakazi Nchini
May 01, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi wetu-MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha maslahi ya Wafanyakazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo kupunguza kiwango cha kodi kwa wafanyakazi, kuongeza umri kwa watoto katika huduma za bima ya afya, tozo ya asilimia 6 ya elimu ya juu, kupandisha vyeo kwa watumishi, kulipa malimbikizo ya Watumishi na ajira mpya.

Rais ameyasema hayo leo wakati wa maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) yaliyofanyika katika uwanja wa jamhuri jijini Dodoma na kusema kuwa kama Serikali ingetangaza kiasi cha mshahara kwa mwaka 2021 kisingefika kiwango cha fedha ambacho serikali imeziacha kwa watumishi kwa kupunguza kodi, tozo na marekebisho kwenye huduma mbalimbali.

“Serikali imejitoa kupandisha maslahi ya mfanyakazi kwa kupunguza kiwango cha PAYE ile kodi ya mshahara kwa punguzo lile serikali ilisamehe kukusanya zaidi ya Bilioni 14 ambazo zilibaki kwa wafanyakazi lakini pia tuliongeza umri wa bima toka miaka 18 ya watoto hadi miaka 21 pia tozo ya asilimia 6 ya Elimu ya juu pamoja na tozo ya adhabu ya kuchelewa kulipa ya asilimia 10. Kwa kuisamehe mwaka mmoja Serikali imesamehe billion 50”

“Lakini pia tulipandisha vyeo kwa Watumishi 198,215 ambapo kupanda vyeo huko kumeendana na kupanda kwa mishahara yao na Serikali ilitumia bilioni 41, tulifanya ubadilishwaji wa kada au miundo ya utumishi milioni 4.3 lakini pia tulilipa malimbikizo ya watumishi 75,007 shilingi billion 124.3 zilitumika lakini vilevile tulitoa ajira mpya ambapo serikali ilibidi kutumia shilingi bilioni 1na milioni 100. Fedha zote hizo zilibaki kwenu wafanyakazi” amefafanua Rais Samia.

Aidha, akizungumza kuhusu Watumishi wa darasa la 7 walioondolewa pamoja na mkumbo wa vyeti feki na wale wote waliofanya kazi kwa muda mrefu wakafukuzwa kwa ajili hiyo, Rais Samia ameagiza Wizara ya Fedha kuanga ni kiasi gani wafanyakazi walikatwa kwenye jasho la mishahara yao ili waweze kulipwa.

Mbali na hayo, Rais Samia ameagiza Waajiri kuhakikisha taarifa za wastaafu zipo sahihi kwenye mifuko miezi sita kabla ya mtumishi kustaafu ili kuweza kufanikisha stahili za Wataafu kwa wakati.

“Kwa kuwa taarifa za Wafanyakazi kustaafu huwa zinajulikana kabla ya miezi 6, ninawaagiza Waajiri waandae malipo ya Wastaafu wanaotarajia kabla ya tarehe ya kustaafu pia kuhakikisha taarifa za Watumishi hao ziko kikamilifu katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii” amesisitiza Rais Samia.

Sambamba na hilo, Rais Samia ameiagiza Viongozi wa Mkoa na Wilaya kuweka utaratibu wa kuwapanga Wamachinga na waendesha pikipiki ili waweze kufanya shughuli zao za kujiingizia kipato.

“Viongozi wa Mkoa na Wilaya twendeni na maelekezo wekeni utaratibu wa kuwapanga Wamachinga na sio kuwazuia kufanya shughuli zao za kujiingizia kipato, nimeshaletewa malalamiko kutoka baadhi ya sehemu na naendelea kuyafanyia kazi, nataka viongozi mtumie busara zaidi kuliko mabavu katika kushughulikia kero za wananchi” amesisitiza Rais Samia

Huu ni mualiko wa pili kwa Rais Samia kushiriki maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani kama mdeni rasmi toka kuapishwa kwake kama kama kiongozi wa taifa la Tanzania.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi