Serikali ya Awamu ya Sita imetoa jumla ya shilingi bilioni 10.8 kwa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa jengo jipya la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD).
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki Ulisubisya ameyasema hayo leo Machi 03, 2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa ni programu iliyoandaliwa na Idara hiyo.
“Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa jengo jipya la kuhudumia wagonjwa wa nje umefikia asilimia 14, tunatarajia mradi huu ukikamilika utapunguza msongamano wa wagonjwa katika OPD ya sasa kwani zaidi ya wagonjwa 1,500 wataweza kuhudumiwa kwa siku”, amesema Dkt. Ulisubisya.
Ameongeza kuwa, Serikali imetoa fedha zaidi kwa ajili ya miradi mingine ikiwemo mradi wa upanuzi wa eneo la kutolea huduma uliofikia asilimia 78 ambapo Taasisi ya MOI inafanya ukarabati wa iliyokuwa hospitali ya Tumaini kuwa sehemu ya MOI ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa nje. Mradi huo unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.5 na utawezesha wagonjwa wengi kuhudumiwa kwa urahisi.
"Pia Serikali imekamilisha kwa asilimia 100 ujenzi wa ‘oxygen plant’ kwa gharama ya shilingi 1,675,893,448.84, kukamilika kwa ujenzi huo kutaisaidia Taasisi ya MOI kuokoa shilingi 1,150,000.00 kwa siku ambazo zilikua zinatumika kununua hewa ya Oksijeni" ameongeza Dkt. Ulisubisya
Maboresho mengine yaliyofanywa kupitia fedha za Serikali ni pamoja na ukarabati wa wodi za kulaza wagonjwa pamoja na maeneo mengine ya kutolea huduma.
Vile vile, Serikali inatarajia kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya muda mrefu ikiwemo mradi wa kimkakati wa ujenzi wa hospitali ya kisasa ya utengamao Mbweni pamoja na kuanza kwa taasisi ya sayansi ya mishipa ya fahamu na ubongo (Tanzania Neuroscience).
Dkt. Ulisubisya amewahakikishia Watanzania na raia wa nchi nyingine za Afrika kuwa, MOI itaendelea kutoa huduma bora na kuwaondolea adha ya kufuata huduma nje ya nchi.