Mkurugenzi Mkuu, Tume ya Taifa na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu amesema kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, serikali imetenga shilingi bilioni 6.3 kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Nungu amesema hayo leo Machi 17, 2025 katika Ofisi za Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa tume hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Serikali imetenga shilingi bilioni 6.3 kwa ajili ya miradi ya utafiti wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku shilingi milioni 600 zikielekezwa katika miradi minne ya usalama wa chakula, ikihusisha udhibiti wa magonjwa ya mazao, uboreshaji wa uhifadhi wa chakula na ubunifu wa vyakula vyenye virutubishi vya hali ya juu,” amefafanua Dkt. Nungu.
Ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita kuwa ni pamoja na serikali kutoa fedha na kuweka mazingira rafiki kwa wanasayansi na wabunifu wa Kitanzania.
“Kupitia mfumo wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali ya Tanzania na nchi rafiki pamoja na taasisi za kimataifa, COSTECH imepokea shilingi bilioni 5.65 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya utafiti wa pamoja kati ya watafiti wa Tanzania na washirika wetu,” amesema Dkt. Nungu.
Vilevile COSTECH imeanzisha na kuziwezesha kongano nane bunifu katika mikoa ya Kigoma, Geita, Mafia, Mbeya, Dodoma, Morogoro, Singida na Pemba ili kusaidia sekta ya viwanda na kilimo.
Dkt. Nungu amesema miradi hiyo imewezeshwa kwa ufadhili wa shilingi milioni 750, kuhakikisha teknolojia bora zinatumika katika kuboresha uzalishaji wa mafuta ya mawese, dhahabu na mazao ya baharini.
“Kwa kuwekeza shilingi bilioni 2.3 kupitia Samia Commercialization Fund, serikali imewapa wabunifu wa Kitanzania fursa ya kuingiza bunifu zao sokoni, hii inasaidia kuondoa changamoto ya kukosekana kwa dhamana ili kupata mitaji,” amefafanua Dkt. Nungu.
Sambamba na hayo COSTECH imefanikiwa kuandaa mifumo ya usimamizi wa tafiti kwa kutumia teknolojia za kidijitali kupitia mradi wa HEET, pamoja na kuanzisha vigoda vya utafiti katika vyuo vikuu kama SUA na NM-AIST kwa ufadhili wa shilingi bilioni 4.7.
“Kwa mafanikio haya, Tanzania inajiweka katika nafasi ya ushindani wa kimataifa katika nyanja ya sayansi na teknolojia. Uwekezaji huu si wa kawaida, bali ni hatua ya kimkakati inayoonesha kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu ameleta mapinduzi katika sekta ya sayansi na teknolojia, ikiwa ni kielelezo cha uongozi wenye dira na maono makubwa kwa taifa,” amesema Dkt. Nungu.