Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yatekeleza Miradi ya Maji 9 Bunda
Mar 06, 2025
Serikali Yatekeleza Miradi ya Maji 9 Bunda
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA), Bi. Esther Gilyoma, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita leo tarehe 6 Machi, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mji wa Bunda, imetekeleza jumla ya miradi ya maji tisa ambapo kati yake, miradi minne imekamilika kwa asilimia 100 na mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA), Bi. Esther Gilyoma ametoa takwimu hizo leo Machi 06, 2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari- MAELEZO jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa Mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa ni programu iliyoandaliwa na Idara hiyo.

Bi. Esther amesema kuwa, mnamo mwaka 2021 maji yaliyokuwa yanazalishwa ni wastani wa meta za ujazo 2,976 kwa siku na kwa sasa maji yanayozalishwa ni wastani wa Meta za ujazo 5,160 kwa siku ambapo uzalishaji huo wa maji unaendelea kuongezeka siku kwa siku kutokana na mahitaji na upanuzi wa mtandao wa bomba unaondelea kufanyika.

“Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024, imetekeleza mradi wa ujenzi wa chujio la maji Nyabehu – Bunda uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 10.6 ambao tayari umekamilika na unahudumia wananchi 227,446, pia umetekeleza mradi wa miundombinu ya majitaka Butakale – Bunda kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7 ambao kwa sasa umefikia asilimia 46 ya utekelezaji wake”, amesema Bi. Esther.

Ametaja miradi mingine iliyokamilika ikiwemo ya ujenzi wa maji Balili, Rubana na Kunzugu – Bunda uliojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 759.9, mradi wa ujenzi wa maji Manyamanyama Mugaja – Bunda kwa gharama ya shilingi bilioni 1.1 na mradi wa ujenzi wa maji Misisi- Zanzibar Mjini Bunda kwa gharama ya shilingi milioni 733.2.

Vile vile, ameitaja miradi inayoendelea na utekelezaji kuwa ni mradi wa kusambaza maji Wariku wa shilingi bilioni 1.6 ambao umefikia asilimia 40, mradi wa kusambaza maji Kisangwa unaogharimu shilingi milioni 716.1, mradi wa kusambaza maji Migungani Kaswaka unaogharimu shilingi bilioni 1.3 na mradi wa kusambaza maji Nyamswa Bunda unaogharimu shilingi bilioni 8.4.

Kwa sasa inakadiriwa kuwa, eneo linalohudumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira- Mji wa Bunda lina wakazi 195,848 (2024) kati ya hao, asilimia 85 % ambayo ni sawa na wakazi 165,613 ndio wanapata huduma ya maji ya bomba hivi sasa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi