Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yataja Maeneo 10 ya Kipaumbele Kwenye Uwekezaji
Dec 08, 2025
Serikali Yataja Maeneo 10 ya Kipaumbele Kwenye Uwekezaji
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari kuhusu mikakati ya Wizara yake kuzalisha ajira nyingi kwa vijana kupitia Uwekezaji unaofanyika hapa nchini katika kipindi cha miaka mitano ijayo leo Desemba 8, 2025 jijiji Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu – MAELEZO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo ametangaza maeneo 10 yanayopewa kipaumbele katika uwekezaji na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuzalisha ajira milioni nane na kuvutia mtaji wenye jumla ya dola za Kimarekani bilioni 50 ifikapo 2030

Prof. Mkumbo amesema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari, jijini Dar es salaam, Desemba 8, 2025 kuelezea mwelekeo wa Serikali katika kuimarisha na kuvutia uwekezaji katika kipindi cha miaka 5 ijayo ambapo amesema Serikali itaweka mkazo katika shughuli za kilimo, uvuvi, viwanda, mifugo, utalii, ujenzi wa majengo, madini, huduma za fedha, misitu na nishati ikiwemo mafuta na gesi.

Amesema kupitia uwekezaji huo, Serikali itaongeza fursa za ajira, kupanua na kukuza mitaji ya uwekezaji na kuweka mikakati ya kuimarisha shughuli za kilimo na uchakataji wa mazao ya kilimo kwa kuzingatia umuhimu wake katika kukuza kipato kwa kuwa asilimia 66 ya Watanzania wanategemea sekta hiyo kuendesha maisha yao.

Prof. Mkumbo ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 5 ijayo, Serikali itaweka mkazo katika uzalishaji wa bidhaa muhimu kwa matumizi ya ndani na zile ambazo zimekua zikiagizwa zaidi kutoka nje nchi kama vile dawa na vifaa tiba, mafuta ya kupikia na ngano.

Amesema Serikali itaendelea kukaribisha, kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji katika kujenga kiwanda cha kukamua mafuta ya kupikia, kuanzisha vitalu vya kuzalisha mbegu bora za mafuta ya kula, kuanzisha mashamba makubwa ya kulima alizeti na ngano pia kujenga viwanda vya kutosha ili kuwe na upatikanaji wa malighafi na viwanda vya uchakataji wa mafuta kwa lengo la kuifanya Tanzania ijitegemee kwa kupunguza matumizi ya fedha za kigeni nje ya nchi.

“Mwaka 2024 tulitumia trilioni 14 kuagiza bidhaa 96 kutoka nje ya nchi. Tumeangalia kati ya bidhaa hizo nyingi tunaweza kuzizalisha hapa ndani kufuatia viwanda vyetu vingi kupanuliwa vikiwemo vya sukari. Kuanzia mwaka 2026 hatutaagiza tena sukari kutoka nje ya nchi;   tumeweka mkazo kwenye mafuta ya alizeti ambayo pia yamekua na uhitaji mkubwa ndani na nje nchini” amesisitiza Prof. Mkumbo.

Aidha, Prof. Mkumbo amesema Serikali itaendelea kuimarisha na kuanzisha malisho ya mifugo, ranchi za biashara pia kuimarisha shughuli za uvuvi na ufugaji wa Samaki kwa kuanzisha viwanda zaidi vya kuchakata Samaki.

“Hili ni eneo ambalo Serikali tumeona tuliwekee mkazo wa uwekezaji. Tunataka maeneo yetu yajiendeshe kibiashara, Tanzania ni wa pili Afrika kwa kuwa na mifugo mingi, tunataka tuwe na viwanda vitakavyochochea uwekezaji zaidi na ajira kwa watu wetu” amesema Prof. Mkumbo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi