Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yasikitishwa Kushambuliwa kwa Wanahabari
Apr 24, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Nuru Juma

Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari katika mvutano uliotokea juzi jijini Dar es Salaam kati ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana za Chama cha Wananchi (CUF).

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi, idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi katika taarifa yake aliyoitoa leo tarehe 24 Aprili, 2017 kwa vyombo vya habari.

 “Tumechukua muda kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini licha ya baadhi ya waandishi kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo ambao vifaa vyao vya kazi vililengwa katika shambulizi hilo”. Alisema Dkt. Abbasi

Aliongeza kuwa Serikali imelaani kitendo cha kuumizwa kwa wanahabari hao ambao walikuwa wamealikwa kuhudhuria mkutano huo.

“Ifahamike kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii”. Alisisitiza Dkt. Abbasi.

Pia Dkt. Abbasi aliaanisha baadhi ya vifungu vya Sheria vinavyomlinda mwanahabari katika kazi yake ambapo kifungu cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa.

Aliongeza kuwa misingi ya uhuru huo wa kitaaluma umesisitizwa pia  katika Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na  Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu imeuridhia hivyo wananchi wanatakiwa kuheshimu hilo.

Dkt. Abbasi aliwatakia nafuu ya haraka wanahabari waliojeruhiwa na wengine waliopatwa na jakamoyo katika tukio hilo na kuwaomba wadau wote wa habari na wanasiasa kutulia na kuviachia vyombo husika vifanye kazi yake ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi