Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yashauriwa Kuanzisha Viwanda vya Kurejeresha Taka Ngumu na Zinazooza.
Jun 06, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Jovin Mihambi.

Serikali imeshauriwa kuanzisha viwanda vya kurejeresha taka (recycling) ili kuongeza ajira kwa wanachi pamoja na kudhibiti uchafuzi wa mazingira ambao unasababisha uharibifu mkubwa kwa viumbe hai katika Ziwa Victoria pamoja na mahali pengine nchini.

Hayo yamesemwa na wadau wa mazingira wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza katika maadhimisho ya kilele cha siku ya mazingira  Duniani, Juni 5.

Wadau hao wamesema kuwa Serikali inayo fursa ya kuanzisha viwanda hivyo kutokana na kuwepo kwa uwingi wa taka ngumu na zile  zinazozalishwa kutoka viwandani, majumbani na sehemu mbalimbali  ambazo hutupwa katika madampo huku zikiwa na thamani kubwa endapo zingerejereshwa na kufanyia kazi nyingine.

Mwezeshaji wa warsha hiyo, kutoka katika Shirika la Kimataifa la Swisscontact Tanzanian lenye makazi yake jijini Mwanza, Patric Matandala alisema, imefika wakati Serikali ya Tanzania iweze kutambua kuwa taka ni mali na endapo itaweza kuanzisha viwanda hivyo, itatengeneza ajira kubwa kwa wananchi na kuongeza pato la Taifa.

Aliendelea kwa kusema kuwa wananchi wakipewa elimu ya kutosha jinsi ya kutambua taka ngumu na zile zinazooza watatumia  fursa hiyo ya kukusanya taka na kuziuza viwandani badala ya kuzitupa.

"Wenzetu kutoka nchi zilizoendelea huwezi kuwaona wakitupa taka kwa sababu wanatambua kuwa taka ni mali", alisema Matandala.

Nae, Joyce Ndesamburo ambaye ni mdau wa mazingira alisema, uchumi wa viwanda utakuwa na manufaa makubwa kama Serikali itatoa elimu juu ya umuhimu wa urejereshwaji wa taka ngumu na zile zinazooza kwa kuanzia ngazi ya kaya, mtaa hadi mkoa.

Alisema, baadhi ya wananchi wakiona mtu anaokota chupa za plastiki kwa ajili ya kwenda kuziuza humuona kama mtu ambaye hana hustaarabu. Hivyo amewataka watu wenye dhana hiyo kujirekebisha na kuziona taka kuwa ni mali.

Aidha, washiriki wa warshsa hiyo wameiomba Serikali kufanya utafiti wa kina katika  majiji, manispaa, halmashauri za wilaya pamoja na wadau ambao ni wananchi ili kubaini kiasi cha tani zinazozalishwa kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya kurejesha taka hapa nchini.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi