Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yasaidia Wajasiriamali Zaidi 300 Kushiriki Maonesho ya Juakali Uganda
Dec 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikisha ushiriki wa Wajasiriamali zaidi ya 300 katika maonesho ya 22 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Wajasiriamali Wadogo na Wakati maarufu Juakali yanayofanyika katika viwanja vya Uhuru vya Kololo jijini Kampala, Uganda kuanzia terehe 8 - 18 Disemba 2022.

Maonesho hayo yanayongozwa na kauli mbiu “Nunua Bidhaa za Afrika Mashariki, ili kujenga Uchumi Stahimilivu na Endelevu wa Afrika Mashariki” yanalenga kutoa fursa kwa Wajasiriamali ya kuonesha huduma na bidhaa mbalimbali wanazozalisha na kubadilishana uzoefu, ujuzi na taarifa na wajasiriamali wenzao katika Jumuiya sambamba na kukuza wigo wa masoko mapya.

Maonesho hayo ambayo yamevutia Wajasiriamali zaidi 1,500 kutoka Nchi zote saba (7) Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo ikikadiriwa 75% kati yao kuwa ni wanawake, yamesheheni bidhaa mbalimbali zenye asili ya Jumuiya. Kwa upande wa wajisiliamali wa Tanzania miongoni mwa bidhaa na huduma wanazozionesha ni pamoja na mavazi ya asili, bidhaa za baharini, bidhaa za kilimo zilizoongezewa thamani, mashine za kuzalisha bidhaa mbalimbali, madawa ya asili, vito vya thamani na madini, utalii, na bidhaa za ngozi kama vile viatu, mabegi na mikoba. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wajasiriamali wa Tanzania wameonesha kuridhishwa kwao na kupongeza juhudi na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania chini ya uongozi madhubuti wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kushiriki katika maonesho hayo. 

“Kutokana na gharama kubwa za kusafirisha bidhaa zetu hadi hapa nchini Uganda, wengi wetu tusingeweza kumudu, hivyo tusingeweza kuwa na uwakilishi wa kutosha katika maonesho haya. Hata hivyo kutokana na dhamira ya Serikali ya kutusaidia wajasiriamali kukua kibiashara kupitia kupata masoko mapya ya huduma na bidhaa tunazozalisha na kutuongezea ujuzi na uzoefu imeona ni vyema ituwezeshe katika maeneo mbalimbali ikiwemo kugharamia usafiri wa kutuleta hapa nchini Uganda na kuturudisha nyumbani baada ya maonesho”. Ameeleza Lilian Sambu mjasiriamali. 

Maonesho ya Juakali yalifanyika kwa mara ya kwanza mwezi Novemba 1999 jijini Arusha, ambapo yaliambatana na tukio la kihistoria la kusainiwa kwa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika maonesho hayo, Wakuu wa Nchi za Jumuiya Afrika Mashariki walielekeza kuwa yafanyike kila mwaka kwa mzunguko kati ya Nchi Wanachama ili kuimarisha mtangamano wa jamii na uchumi wa watu wa Afrika Mashariki.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi