Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yapongezwa Ushirikishwaji Wananchi Maboresho Sera ya Uwekezaji, Ukusanyaji Mapato
Feb 28, 2024
Serikali Yapongezwa Ushirikishwaji Wananchi Maboresho Sera ya Uwekezaji, Ukusanyaji Mapato
Siku ya Pili ya Jukwa la Kodi na Uwekezaji 2024 likiendelea, leo tarehe 28 Februari kwenye ukumbi wa JNICC Dar es salaam
Na Lilian Lundo - Maelezo

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa namna inavyoshirikisha wananchi katika maboresho ya sera ya uwekezaji na ukusanyaji wa mapato.

Pongezi hizo zimetolewa leo Februari 28, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam linapofanyika Jukwaa la Kodi na Uwekezaji 2024.

“Kwa uwepo wa Makamu wa Rais jana, na viongozi wa serikali leo, tumeona serikali yetu sikivu ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inavyoweza kuwaweka karibu wananchi wake kupitia wawakilishi wake kutoa mawazo na maoni, ili kurekebisha katiba na sheria zetu za nchi, na tuweze kwenda pamoja. Huu ndio uongozi ambao tulikuwa tukiulilia siku zote,” amesema Mshauri wa Kodi Auditax International, Bw. Sylivester Ntungu.

Aidha Bw. Ntungu amependekeza serikali kuendelea kuhusisha wananchi kama ambavyo inavyowahusisha sasa, ili waweze kuwasilisha masuala ambayo yatainua uchumi wa nchi na kuondoa changamoto mbalimbali ambazo wanakumbana nazo katika uendeshaji wa shughuli zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Geo Planning, Leonard Bamhig amesema, “tumefurahi kuona kuna nia ya dhati ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, wametuhusisha sisi kama wadau, na tumeona nia ya serikali kwamba sasa inahitaji kuinua sekta binafsi, ili sekta hii iwe na mchango mkubwa katika nchi, lakini kuinuliwa sisi kama wafanyabiashara wa Kitanzania kuwa mojawapo kati ya watu watakaohusika katika kukuza uchumi wetu”.

Jukwaa la Kodi na Uwekezaji 2024, lilifunguliwa Februari 27, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ambapo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Kitila Mkumbo pamoja na wafanyabiashara mbalimbali.

Jukwaa hilo linabebwa na kauli inayosema, “maboresho ya sera katika uwekezaji, ukusanyaji wa mapato ya ndani na ukuaji wa uchumi jumuishi”.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi