Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yapongeza Juwanata kwa Kuanzisha Jumuiya ya Wasindikaji Nafaka
Oct 30, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na: Mwandishi Wetu

Serikali imeupongeza uongozi wa muda wa Jumuiya ya Wasindikaji Nafaka Tanzania (JUWANATA) kwa kukamilisha rasimu ya katiba ya umoja  wao

Pongezi hizo za serikali zimetolewa leo na Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Masoko toka Wizara ya Kilimo Benito Kavenuka wakati wa mkutano maalum wa Juwanata uliofanyika Jijini Dar es Salaam .

Kavenuke amesema kuundwa kwa jumuiya ya wasindikaji mazao ya nafaka ni utekelezaji wa azimio la mkutano wa wafanyabiashara ya mazao ya nafaka uliofanyika mwezi Agosti mwaka huu chini ya  Waziri wa Kilimo.

“Serikali inaunga mkono Juwanata kwa kutekeleza kwa haraka azimio la mkutano wa Waziri wa Kilimo na wafanyabiashara wa nafaka la kuanzisha jumuiya hii muhimu  kwa ustawi wa viwanda vya mazao ya nafaka.” alisema Kavenuka.

Aliongeza kusema serikali itapenda kuona Viongozi wa jumuiya hii wanasimamia viwango vya ubora wa bidhaa za nafaka  zinazalishwa ili kuwa na uhakika wa soko na bei nzuri.

Kavenuka amewataka pia kuongeza wigo wa kuwafikia wasindikaji waliopo mikoani kujiunga na jumuiya hii,ili serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo iwe rahisi kutoa huduma za kukuza sekta ya usindikaji nafaka nchini.

Akitoa taarifa ya mkutano huo maalum,Mwenyekiti wa muda wa Juwanata Oscar Munisi alisema lengo la jumuiya  ni kuitikia kwa vitendo kauli mbiu ya serikali ya kujenga viwanda vya kuongeza thamani mazao ya nafaka .

 Munisi aliongeza kusema jumuiya yao inaundwa na wanachama wamiliki wa viwanda vya kusindika nafaka na mafuta toka mikoa yote ya Tanzania bara ambapo kazi ya kuandaa katiba ya muda ilishirikisha wadau wote

“Tunataka kuwa na Katiba itakayosaidia kusajili wasindikaji wote nchini hususan wajasiliamali wadogo ili tuwe na sauti ya pamoja katika kuyafikia masoko ya bidhaa za nafaka kwa ushirikiano na serikali” alisema Munisi

Alitaja changamoto ya  wajasiliamali wasindikaji kwa sasa nchini kuwa ni kufikia masoko kama ya  Lubumbashi Kongo imekuwa ngumu kwa kukosekana chombo cha kuwaratibu.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Baraza la Nafaka la Afrika Mashariki (EAGC) Ikunda Terry amewataka wasindikaji hususan wa mchele   kuongeza ubora ili kufikia soko  kubwa la nchi za Uarabuni.

“Tanzania ina fursa ya soko la uhakika la mchele kwani sasa uzalishaji  umefikia tani 2,200,000  wakati matumizi  ya ndani kwa mwaka ni kama tani milioni moja,kwa hiyo tunayo ziada ya zaidi ya tani milioni moja kwa ajili ya kuuza  nje ya nchi” alisisitiza Ikunda.

Kufanyika kwa mkutano huu maalum kunafatia mkutano wa Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga alioitisha hapo tarehe 29 na 30 Agosti mwaka huu kujadili changamoto za masoko ya mazao ya nafaka nchini.

Mwisho.

Imeandaliwa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Kilimo

Dar es Salaam

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi