Na Ramadhani Kissimba na Saidina Msangi, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amepokea kiasi cha shilingi bilioni 4.5 kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) zikiwa ni gawio kwa Serikali kutokana na faida iliyopata Benki hiyo mwaka 2020/21.
Akizungumza katika hafla fupi ya kupokea gawio hilo iliyofanyika Jijini Dodoma, Mhe. Dkt. Nchemba aliipongeza Benki hiyo kwa kuendelea kuimarika na kuongeza faida kila mwaka inayosababisha kuongezeka kwa kiwango cha kodi kinacholipwa Serikalini na gawio linalotolewa kwa Wanahisa wote ikiwemo Serikali ambayo ina hisa ya asilimia 30 katika Benki hiyo.
"Nimefarijika sana kusikia kuwa kwa mwaka 2021 Benki ya NBC ilipata faida kabla ya kodi ya shilingi bilioni 60, ambalo ni ongezeko la asilimia 702 kutoka faida ya bilioni 6.2 iliyopatikana mwaka 2020. Haya ni mafanikio makubwa sana" alisema Mhe. Nchemba.
Mhe. Nchemba aliongeza kuwa ni jambo la kujivunia kuona kuwa Serikali ambayo ina umiliki wa asilimia 30 ya hisa za Benki ya NBC, inapata kiasi cha shilingi bilioni 4.5 kama gawio lake, pesa ambazo zitatumika kugharamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini na kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na maji.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru, alisema kuwa kutolewa kwa gawio hilo kutoka NBC inathibitisha kuwa maamuzi yaliyofanywa na Serikali katika kubinafsisha Mashirika ya Umma yalikuwa ni maamuzi yenye tija ambayo sasa yanatoa mchango mkubwa wa kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Aidha, Bw. Mafuru alizitaka Taasisi zinazomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kujifunza kutoka kwenye mashirika yanayomilikiwa kwa ubia na Serikali ili kuona ni jinsi gani yatajiendesha kwa faida.
Bw. Mafuru alisema kuwa sekta ya Benki nchini kwa sasa imekua kwa asilimia 10 hivyo kusababisha sekta hiyo kuwa Taasisi muhimu inayogharamia shughuli za Uchumi nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw. Theobald Sabi, aliishukuru Serikali kwa kuiwezesha Benki hiyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji na kueleza kuwa mwaka 2021 Benki hiyo imetoa kodi shilingi bilioni 20 serikalini Pamoja na kutoa gawio hilo la sh. Bilioni 4.5.
Alisema pia kuwa Benki yake imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni moja (1) iliyotumika katika misaada ya kijamii, na uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 9 zilizotolewa kwenye mchezo wa soka kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia msimu huu wa ligi na NBC Premier league..
Bw. Sabi, alisema uwekazaji huo uliofanywa na NBC umezalisha ajira zaidi ya elfu tisa (9) na ajira zaidi zinaendelea kutolewa kutokana na mnyororo wa thamani kupitia sekta ya michezo.
Naye Kaimu Msajili wa Hazina ambaye Ofisi yake inasimamia mashirika ambayo Serikali imewekeza hisa zake pamoja na mashirika ambayo inamiliki hisa chache, Bw. Joseph Mwaisemba alisema kuwa hadi kufikia mwezi Mei, Ofisi yake ilifanikiwa kukusanya maduhuli yai kiasi cha shilingi bilioni 691 na inahitaji kiasi cha sh. bilioni 86 ili iweze kufikia lengo na kwamba gawio hilo la NBC linapunguza nakisi hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Sillo, aliipongeza NBC kwa kutoa gawio hilo pamoja usimamizi mzuri wa Serikali uliosababisha kupatikana kwa gawio hilo ambalo litasaidia kufanikisha utekelezaji wa miradi ya Serikali iliyolenga kuwanufaisha wananchi katika nyanja mbalimbali.
Akihitimisha maelezo yake katika hafla hiyo, Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amewataka Watanzania kujiandaa na kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika tarehe 23 Agosti, 2022. Mhe. Nchemba amewakumbusha wananchi kuwa Sensa ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi hivyo wajiandae kuhesabiwa.