[caption id="attachment_37017" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Saza kilichopo wilayani Songwe mkoani Songwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 18 Oktoba, 2018.[/caption]
Na Greyson Mwase, Songwe
Serikali kupitia Wizara ya Madini imepiga marufuku usafirishwaji wa kaboni kwa ajili ya kuchenjulia madini ya dhahabu kutoka mkoa mmoja hadi mwingine na kusisitiza kuwa haitasita kumchukulia hatua za kisheria mchimbaji wa madini atakayekiuka agizo hilo.
Agizo hilo limetolewa leo tarehe 18 Oktoba, 2018 na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo katika mkutano wake na wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Saza kilichopo wilayani Songwe mkoani Songwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.
Katika ziara yake Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremeah, Afisa Madini Mkazi katika Mkoa wa Mbeya, Sabai Nyansiri, Afisa Madini anayesimamia wilaya za Songwe na Chunya, Athuman Kwariko, Maafisa Madini kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mbeya, Ndege Bilagi na Mhandisi Godfrey Nyanda, vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya pamoja na waandishi wa habari.
Akizungumza na wachimbaji hao, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa lengo la Serikali kupitia Wizara ya Madini kupiga marufuku usafirishwaji wa kaboni kutoka katika mkoa mmoja kwenda mwingine tangu Juni mosi mwaka huu lilikuwa ni kuhakikisha kila mkoa unapata mapato stahiki kupitia ujenzi wa mitambo ya kuchenjua madini kwa kutumia kaboni.
[caption id="attachment_37018" align="aligncenter" width="750"] Msimamizi wa uchimbaji madini katika Mgodi wa Dhahabu wa Sunshine uliopo katika kijiji cha Mbangala wilayani Songwe mkoani Songwe, Evarist Lukuba (kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa tatu kushoto mbele) mara alipofanya ziara katika mgodi huo.[/caption]“Kama Serikali tunataka kuhakikisha kila mkoa unajenga mitambo ya kuchenjua madini badala ya kwenda kuchenjulia katika mikoa ya jirani kwa kutumia kaboni na kukosa mapato stahiki,” alifafanua Nyongo.
Alisisitiza kuwa, Serikali haitasita kutaifisha kaboni itakayokamatwa ikisafirishwa kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine ikiwa ni pamoja na kuwachukulia wahusika hatua za kisheria.
Akielezea mikakati ya Wizara ya Madini katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini, Nyongo alisema kuwa Wizara imeshaanza kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchini na kuwataka kuunda vikundi na kuomba leseni ili waweze kufanya shughuli zao za uchimbaji wa madini kwa kufuata sheria na kanuni za madini.
Aliongeza kuwa, Wizara ya Madini imeanza kujenga vituo vya umahiri kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu namna bora ya kubaini, kuchimba na kuchenjua madini na kueleza zaidi kuwa moja ya kituo kinachotarajiwa kujengwa ndani ya kipindi cha miezi sita kitakuwa katika Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.
[caption id="attachment_37019" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (mbele) pamoja na msafara wake wakiendelea na ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa New Luika uliopo katika kijiji cha Mbangala wilayani Songwe mkoani Songwe.[/caption]Aidha, Nyongo aliwataka wachimbaji wadogo kuhakikisha wanalipa mrabaha na kodi mbalimbali zinazotakiwa Serikalini na kuwataka maafisa madini nchini kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa mapato hayo.
Pia, aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kuepuka uchenjuaji wa madini kwa kutumia zebaki kwani ina madhara makubwa katika uharibifu wa mazingira na binadamu.
[caption id="attachment_37020" align="aligncenter" width="750"] Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa New Luika uliopo katika kijiji cha Mbangala wilayani Songwe mkoani Songwe, Honest Mrema (wa pili kulia mbele) akielezea majukumu ya mgodi huo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo pamoja na msafara wake mara alipofanya ziara katika mgodi huo.[/caption] [caption id="attachment_37021" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kulia) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mary-Prisca Mahundi, (wa pili kushoto) mara baada ya kuwasili katika Wilaya hiyo kabla ya kuanza ziara yake rasmi.[/caption]Akielezea namna bora ya usimamizi wa viwanda vitakavyojengwa kwa ajili ya kuchenjua madini ya dhahabu kwa kutumia kaboni, Nyongo alisema mbali na kuhakikisha wamiliki wanakuwa na leseni za uchenjuaji wa madini, wataalam wa mazingira kutoka Wizara ya Madini watapita na kukagua ili kuhakikisha kuwa viwanda vinajengwa katika mazingira mazuri ambayo hayatakuwa na athari katika makazi ya wananchi.
Awali wakizungumza katika mkutano huo kwa nyakati tofauti wachimbaji wadogo waliwasilisha kero mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maeneo kwa ajili ya kuendesha shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, ushuru na tozo nyingi, pamoja na kutoshirikishwa katika mikataba baina yao na wawekezaji wakubwa wa madini.