Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaongeza Uwekezaji Masomo ya Sayansi na Teknolojia .
Jan 31, 2026
Serikali Yaongeza Uwekezaji Masomo ya Sayansi na Teknolojia .
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na mafanikio ndani ya siku 100 za Serikali ya awamu ya Sita; leo Januari 31, 2026, katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Na Grace Semfuko – MAELEZO

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, amesema Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika masomo ya sayansi na teknolojia kwa wanafunzi nchini, ikiwa ni hatua ya kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia yanayoleta mabadiliko makubwa duniani.

Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo leo Januari 31, 2026 Jijini Dodoma, wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa ahadi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na mafanikio yaliyopatikana ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita, muhula wa pili.

Ameeleza kuwa Serikali iliahidi kuwasomesha vijana ndani na nje ya nchi katika masomo ya sayansi, teknolojia na hisabati, na kabla ya kutimia kwa siku 100 za ahadi hiyo, utekelezaji wake tayari umeanza.

“Vijana 16 kati ya 50 waliofanya vizuri zaidi tayari wamechaguliwa na wanaondoka kwenda nchini Afrika Kusini kusomea masomo ya data sayansi, akili unde na fani zinazohusiana na sayansi ya kisasa. Tayari tuliwaaga jana na wanatarajiwa kuondoka kesho. Haya yote yamefanyika kabla ya siku 100 za ahadi ya Rais Samia kumalizika,” amesema Profesa Mkenda.

Amefafanua kuwa uamuzi wa kuwapeleka vijana hao nchini Afrika Kusini umetokana na uwepo wa vyuo bora vinavyotoa mafunzo ya kiwango cha juu katika masomo ya sayansi, uhandisi na teknolojia, sambamba na kuwa na muunganiko mzuri kati ya elimu ya darasani na mahitaji halisi ya soko la ajira.

“Johannesburg kuna vyuo vinavyofundisha kwa ubora masomo ya sayansi, uhandisi na data sayansi, na zaidi vina ushirikiano wa karibu na makampuni ya teknolojia. Hivyo, vijana hawa 16 waliomaliza kidato cha sita hawatapata tu elimu bora, bali pia watapata fursa ya kujifunza kwa vitendo na kufanya kazi katika makampuni ya teknolojia,” ameongeza.

Amesisitiza kuwa vijana hao ni sehemu ya wanafunzi 50 ambao Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliahidi Serikali ianze kuwaandaa na kuwapeleka nje ya nchi kusomea masuala ya teknolojia, ikiwa ni mkakati wa muda mrefu wa kujenga rasilimali watu yenye ujuzi unaohitajika katika uchumi wa kisasa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi