Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaongeza Mikopo ya Elimu ya Juu na Kati, Wanafunzi 276,032 Wanufaika Ndani ya Siku 100.
Jan 31, 2026
Serikali Yaongeza Mikopo ya Elimu ya Juu na Kati, Wanafunzi 276,032 Wanufaika Ndani ya Siku 100.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na mafanikio ndani ya siku 100 za Serikali ya awamu ya Sita; leo Januari 31, 2026, katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Na Aron Msigwa - MAELEZO

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB) imeendelea kuongeza kiwango cha mikopo inayotolewa kwa wananfunzi wa elimu ya kati na elimu ya juu akieleza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26 shilingi bilioni 348.77 zimetumika kugharamia wanafunzi  102,800 walioingia mwaka wa kwanza.

Pia amesema Serikali imetumia shilingi Bilioni 348.77 kugharamia wanafunzi 173,232 wanaoendelea na masomo katika ngazi mbalimbali wakiwemo wa shahada ya kwanza 167,362 , shahada za juu 49 na Diploma 58,821.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 31, 2026 jijini Dodoma, Profesa Mkenda amesema mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndani ya kipindi cha siku 100 za muhula wa pili wa uongozi wake.

Ameeleza kuwa Rais Samia aliahidi kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kati ili kuwapa fursa zaidi vijana kumudu gharama za masomo na kutimiza ndoto zao za kielimu. Profesa Mkenda amesema kuwa ndani ya siku 100 hizo, kiwango cha mikopo na idadi ya wanafunzi walionufaika imeongezeka kwa kiasi kikubwa.

“Katika mwaka wa fedha 2025/2026, ndani ya siku 100 za Rais Samia akiwa madarakani, kupitia HESLB tumetoa mikopo kwa jumla ya wanafunzi 276,032 wa shahada ya kwanza, shahada za juu na stashahada, wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea,” amesema Profesa Mkenda.

Ameongeza kuwa Rais Samia ameendelea kuweka mkazo katika masomo ya sayansi na hisabati kwa lengo la kuongeza idadi ya wataalamu wabobezi katika nyanja za sayansi ya data, akili unde, sayansi ya kompyuta na teknolojia za viwanda. Mkazo huo unatekelezwa kupitia Mfuko wa Samia Scholarship unaolenga kusomesha wanafunzi ndani na nje ya nchi.

Profesa Mkenda amesema hadi sasa, kupitia Samia Scholarship na Samia Scholarship Extended, jumla ya wanufaika 3,137 wameshapatiwa ufadhili. Mpango huo umejikita katika kuandaa vijana wenye ujuzi, utaalamu na umahiri katika sayansi, teknolojia, uhandisi, hesabu , elimu ya tiba pamoja na sayansi shirikishi, kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi