Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaokoa Bilioni 149.8 Huduma Mpya za Kibobezi MOI
May 03, 2025
Serikali Yaokoa Bilioni 149.8 Huduma Mpya za Kibobezi MOI
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki Ulisubisiya, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita tarehe 5 Machi, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Dodoma.
Na Adelina Johnbosco, MAELEZO - Dodoma

Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) imefanikiwa kuanzisha huduma zaidi ya 10 za kibobezi zilizowezesha kupunguza  gharama za matibabu.

Hayo yamebainishwa leo Machi 5, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki Ulisubisya jijini Dodoma katika ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO wakati akieleza mafanikio ya taasisi hiyo ndani ya kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Huduma hizo za kibingwa bobezi zaidi ya kumi zilizoanzishwa MOI ni pamoja na; upasuaji na uchunguzi wa ubongo bila kufungua fuvu, upasuaji wa nyonga na magoti wa marudio, upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu, matibabu ya kiharusi kwa kupitia mishipa mikubwa ya damu ya paja, upasuaji wa kunyoosha mgongo uliopinda (Kibiongo), kuondoa uvimbe kwenye ubongo kupitia tundu la pua, huduma ya maumivu sugu ya mgongo, huduma ya wagonjwa maalum na wagonjwa wa kimataifa, huduma ya mkono wa umeme pamoja na utengenezaji viungo bandia kwa teknolojia ya ‘3D’.

Pia, Taasisi ya MOI imeendelea kutoa huduma nyingine za kibingwa bobezi zikiwemo za upandikizaji wa nyonga bandia, upandikizaji wa goti bandia, upasuaji wa magoti kwa njia ya matundu, upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo (Aneurysm), upasuaji wa mfupa wa kiuno, upasuaji wa kichwa kikubwa na mgongo wazi kwa watoto, upasuaji wa ubongo kwa kufungua fuvu pamoja na upasuaji wa mgongo.

“Katika kipindi cha miaka minne, Taasisi ya MOI imefanikiwa kutoa huduma za kibobezi kwa wagonjwa 7,366, gharama za matibabu haya ndani ya nchi zilikuwa shilingi bilioni 68.4 na kama wagonjwa hawa  wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu, jumla ya shilingi bilioni 218.2 zingetumika. Hivyo serikali imefanikiwa kuokoa shilingi bilioni 149.8 ambazo zimetumika katika shughuli nyingine za maendeleo”- Dkt. Ulisubisya.

Pamoja na mafanikio mengine aliyotanabaisha Dkt. Ulisubisya, ameongeza kwamba, katika kipindi cha Awamu ya Sita, Serikali imeiwezesha Taasisi ya MOI kuwa na vifaa vya kisasa ikiwemo mashine za kisasa za kupumulia, vitanda na gari la kubebea wagonjwa, ununuzi wa mashine mpya ya kisasa ya MRI na CT scan, vitanda vya kisasa vya vyumba vya upasuaji, vitanda vya wodini na makabati ya dawa na ya wodini, mashine za mionzi, mashine za kutakasa vyombo vya kuwahudumia wagonjwa pamoja na mashine ya kutolea dawa za usingizi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi