Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yajivunia "Ajira Portal" Miaka 60 ya Muungano
Apr 15, 2024
Serikali Yajivunia "Ajira Portal" Miaka 60 ya Muungano
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Aprili 15, 2024 jijini Dodoma.
Na Ahmed Sagaff - Maelezo

Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inajivunia kuanzisha tovuti ya ajira portal ikisema ni sehemu ya mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Akizungumza leo jijini Dodoma, Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Simbachawene amearifu kuwa tovuti hiyo imeondoa kero ya muungano iliyokuwepo katika kuajiri watumishi wa umma katika serikali yaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Kutokana na kukua kwa teknolojia, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imejenga program ya rununu (Ajira Portal Mobile App) inayopatikana kwenye “PlayStore na ApStore” za simu janja ili kuwarahisishia waombaji fursa za ajira kupata taarifa za uwepo wa fursa za ajira kiganjani mwao.  

"Waombaji wa fursa za ajira wasio na simu janja wanaweza kujisajili kupitia kikao cha Serikali cha *152*00# na kisha kubofya namba 3 (Ajira, Utambuzi) na kisha kuendelea kufuata maelekezo ya namna ya kujisajili," ameeleza Simbachawene.

Pamoja na hilo, Dkt. Simbachawene amefahamisha kwamba serikali imeanza kutumia mifumo ya kidijitali katika kuwatahini watu walioomba ajira katika utumishi wa umma ambapo sasa hufanya majaribio (Aptitude Test) kwa njia ya kompyuta huko huko walipo bila kusafiri.

"Ili kuitatua kero hii ya muungano, Serikali imeweka utaratibu wa muda wa mgao wa ajira uliokubalika kutumika ni asilimia 79 kwa Tanzania Bara na asilimia 21 kwa Tanzania Zanzibar. Utaratibu huu unatekelezwa kwa mujibu wa Waraka wa Serikali wa tarehe 10 Mei, 2013," amesema waziri huyo.

Sambamba na hayo, Dkt. Simbachawene amehabarisha kuwa serikali inatumia mifumo ya TEHAMA katika kupima ufanisi wa watumishi, malipo ya mishahara na mawasiliano katika utumishi wa umma.

"Miongoni mwa taasisi ambazo watumishi wake wamepitia mchakato wa ajira unaoendeshwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Ofisi ya Waziri mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Fedha, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa," ameeleza Simbachawene.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi