Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yajipanga Kuimarisha Mfumo Madhubuti wa Kikatiba na Kisheria
Apr 17, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Jacquiline Mrisho.

Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kuimarisha mfumo madhubuti wa kikatiba na kisheria ili kufanikisha utekelezaji wa sera na mipango kwa maendeleo ya Taifa.

Hayo yamesemwa leo Bungeni  jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb) alipokuwa akiwasilisha Bungeni Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020.

Balozi Mahiga amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha, wizara hiyo itaendelea kuboresha utoaji wa huduma za kisheria kwa Umma  ambapo imeainisha maeneo mahususi ya vipaumbele na kuyawekea mikakati ya utekelezaji.

"Ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele hivyo vitakavyoisaidia nchi kusonga mbele, katika Bajeti ya Mwaka 2019/20 Wizara yangu inaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 55,175,163,302 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo", alisema Balozi Mahiga.

Balozi Mahiga amevitaja baadhi ya vipaumbele vya Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo vikiwemo vya  kukamilisha maandalizi ya Sera ya Taifa ya Sheria kwa ajili ya mambo ya kisheria na utekelezaji wake kuwa; kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya maboresho katika mfumo wa utoaji haki nchini pamoja na kushiriki katika masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa yanayoihusu wizara.

Vile vile kwa upande wa Mahakama ya Tanzania. baadhi ya vipaumbele ni kuanza ujenzi wa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma pamoja na kuendelea na ujenzi wa Mahakama nchini kote zikiwemo Mahakama Kuu mbili zinazoendelea kujengwa mkoani Kigoma na Mara; na kuanza kujenga nyingine katika mikoa ya Morogoro, Mwanza, Dodoma na Singida.

Aidha, Balozi Mahiga ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa vipaumbele vya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/19 vikiwemo vya wananchi kuwa na uhakika kuhusu upatikanaji wa huduma muhimu za kimahakama,, kupatikana kwa ofisi za kudumu za Wizara na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuimarika kwa hali ya upatikanaji wa huduma za kisheria kupitia TEHAMA pamoja na kupatikana kwa  kiasi kikubwa cha fedha na mali nyingi kilichookolewa na kurejeshwa Serikalini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi