Na Georgina Misama – MAELEZO, Arusha
Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali inaipa nafasi kubwa Sekta ya Habari hapa nchini ambapo kwa mara ya kwanza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atahudhuria maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kama mgeni rasmi.
Waziri Nape amesema hayo leo Jijini Arusha alipofungua rasmi maonesho na majadiliano ya Wadau mbalimbali wa Habari kutoka ndani na nje ya Tanzania kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Mei 03.
“ Mtakumbuka katika historia ya harakati za uhuru wa vyombo vya habari, haikuwahi kutokea Rais kuhudhuria sherehe hizo, Rais Samia Suluhu Hassan amevunja historia hiyo, ametupa heshima kubwa sana na ametuonyesha junsi anavyoipenda Sekta hii ya habari”, alisema Waziri Nape.
Aliongeza kuwa Sekta ya habari ni kiungo muhimu katika kuhakikisha jamii inapatiwa taarifa sahihi, kwa wakati na kwa weledi na kusema ni wajibu wa wadau wa sekta ya habari kuziangalia fursa za kihabari zinazoletwa na maendeleo kwa manufaa ya jamii nzima.“ Wanahabari tumepewa kalamu, maana yake tumepewa uwezo wa kuzisaidia jamii zetu”, alisisitiza.
Aidha, Waziri Nape alisema wakati umefika kwa wanahabari kubadilisha mambo ambayo yanawafanya Waafrika wasifaidi rasilimali zao na kuongeza kwamba mijadala itakayoendeshwa katika maadhimisho hayo itatumika vizuri kutafuta ufumbuzi wa changamoto zote ambazo zimejitokeza kwenye majadiliano.
Kwa upande wa katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi alisema kuwa Sekta ya Habari inaendelea kuchangia vyema katika Pato la Taifa, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni muhimu kwa Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuelekea maendeleo ya kidijitali.
“ Kauli mbiu ya mwaka huu inasema ‘uandishi wa habari na changamoto za kidijiti’, ni kaulimbiu muhimu sana kwa Wizara yetu kwani inalenga kuangalia fursa muhimu zinazoletwa na maendeleo ya kidijitali,” alisema Dkt. Yonazi.
Aliongeza kwamba anamshukuru Waziri wa Habari Mawasiano na Teknolojia ya Habari kwa kuifanya Sekta ya habari kuwa imara na watumishi wa Sekta hii kufanya kazi kwa amani na furaha na kuahidi kufanya kazi kwa bidii, lakini pia aliwashukuru wadau wote wa habari kwa kushirikiana katika kufanikisha maandalizi ya mkutano huo.
Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani yameandaliwa na Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, UNESCO, Jukwaa la Wahariri na taasisi mbali mbali za habari ambapo kwa mwaka huu yamefanyika Tanzania na kuhudhuriwa na nchi kadhaa kutoka barani Afrika zimeshiriki.