Serikali yaboresha huduma bingwa bobezi nchini
11/05/2026 Serikali imeendelea kuboresha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi katika ngazi ya rufaa ili kuhakikisha huduma hizo zinapatikana ndani ya nchi.
Baadhi ya huduma za ubingwa bobezi zilizotolewa kwa wagonjwa kuanzia mwaka 2021/2022 hadi Machi 2026 ni pamoja na upasuaji wa moyo wa kufungua kifua, kuzibua mishipa ya moyo, pamoja na upandikizaji na urekebishaji wa mishipa ya damu ya moyo.
Akizungumza leo bungeni Dodoma Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa alisema katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi Machi 2026 Serikali imenunua na kusimika vifaa tiba vya uchunguzi na matibabu ya wagonjwa vyenye thamani ya Shilingi bilioni 241.6, vifaa hivyo ni pamoja na CathLab kutoka moja hadi nne zinazotoa huduma ya kutibu matatizo ya moyo ya dharura.
“Tumeshuhudia siku za karibuni wananchi wengi wakijiuliza kwa nini magonjwa yameongezeka, pamoja na sababu nyingine za mtindo wa maisha na mabadiliko ya tabia nchi, uwezo wetu wa kugundua na kutambua magonjwa umeongezeka sana kufuatia uwekezaji huu mkubwa”, alisema Mhe. Mchengerwa
Mhe. Mchengerwa alisema uwekezaji katika huduma za ubingwa na ubingwa bobezi umewezesha watanzania wengi kupata huduma hizo ndani ya nchi na karibu na maeneo wanapoishi kwa gharama nafuu ambapo awali walikuwa wakizifuata huduma hizo nje ya nchi.
Aidha Mhe. Mchengerwa alisema uwekezaji huo haujawanufaisha watanzania pekee bali wagonjwa kutoka nchi za jirani nao wamevutiwa na huduma nzuri zinazotolewa na hospitali na taasisi nchini hali iliyopelekea kuhudumia jumla ya wagonjwa 26,770 kutoka nchi za Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi, Msumbiji, Kenya, Burundi, Angola, Rwanda, Sudani ya Kusini, Somalia na Uganda.
“Ifahamike kuwa, Mafanikio haya ya Sekta ya Afya katika kipindi cha Awamu ya Sita si takwimu tu za majengo, vitanda, vifaa na huduma zilizoongezeka; ni simulizi ya maisha yaliyookolewa, matumaini yaliyorejeshwa na utu wa Mtanzania uliolindwa”,
“Kama ambavyo Mwalimu Nyerere aliamini kuwa maendeleo ya kweli ni maendeleo ya watu, kama Nelson Mandela alivyotufundisha kuwa heshima ya binadamu ndiyo msingi wa taifa huru, na kama Kwame Nkrumah alivyosisitiza kuwa uhuru lazima uambatane na uwezo wa kujijenga, Serikali imeonesha kwa vitendo kuwa afya bora ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli. Hivyo, kila zahanati iliyojengwa, kila hospitali iliyoboreshwa, kila mama aliyepata huduma salama, na kila maisha yaliyookolewa ni ushahidi kwamba Tanzania inaendelea kujenga taifa lenye afya, usawa, utu na matumaini kwa vizazi vya sasa na vijavyo”, alisema Mhe. Mchengerwa
Mhe. Mchengerwa alisisitiza kuwa, Afya ya mwananchi si gharama, ni uwekezaji; dawa si bidhaa ya kawaida, ni tiba, ulinzi na usalama; taarifa za mgonjwa si makaratasi, ni maisha yanayohitaji uamuzi wa haraka; na ubora wa huduma si anasa, ni haki ya msingi ya Mtanzania.
“Tunaposema tunaboresha sekta ya afya, tunamaanisha tunajenga mfumo unaolinda maisha, unaozuia umaskini, unaotumia teknolojia kuongeza ufanisi, unaoweka heshima ya mgonjwa katikati ya huduma, na unaoimarisha uwezo wa Taifa kujitegemea”,
“Afya iwe haki, dawa zizalishwe ndani ya nchi, huduma ziwe za kidigitali, vituo viwe na ubora unaotambulika, na kila mgonjwa ahudumiwe kwa heshima. Huu si mpango wa kawaida wa kisekta; ni ahadi ya Taifa kwa watu wake kwamba hakuna Mtanzania atakayeachwa nyuma katika kupata huduma bora za afya, na kwamba Tanzania yenye afya bora ndiyo msingi wa Tanzania yenye uchumi imara, utu, matumaini na maendeleo endelevu”, alisema Mhe. Mchengerwa
Mhe. Mchengerwa alisema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Wizara imeendelea kuimarisha huduma za figo nchini kwa kupanua upatikanaji wa huduma za kuchuja damu ambapo jumla ya wagonjwa 3,342 wamehudumiwa. Aidha, katika kipindi hicho, hospitali tatu zimeanza kutoa huduma ya kuchuja damu ikiwemo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na kufanya jumla ya vituo vinavyotoa huduma hiyo kufikia 74.
“Mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza yanahitaji si tiba tu, bali kinga, mabadiliko ya mtindo wa maisha na uelewa wa pamoja kwa jamii. Serikali itaendelea kuwekeza katika afua za kinga na uchunguzi wa mapema katika kudhibiti ukuaji wa magonjwa yasiyoambukiza ili kuepuka gharama kubwa za matibabu kwa wananchi na Serikali”, alisema Mhe. Mchengerwa