Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA. Anthony Kasore amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, jumla ya kiasi cha bilioni 233.7 kimetolewa kwa Mamlaka hiyo kwa ajili ya kuboresha elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
CPA. Anthony Kasore ameyasema hayo leo Machi 03, 2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa ni program iliyoandaliwa na Idara hiyo ya Wakuu wa Taasisi kuelezea utekelezaji wa taasisi zao.
CPA. Kasore amesema kuwa, serikali kupitia Sera, Mipango na Mikakati ya Taifa, (Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023; Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025; Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/2022-2025/2026) imeweka msisitizo kwenye eneo la kutoa na kuendeleza ujuzi kwa ajili ya kuandaa nguvu kazi itakayoshiriki katika maendeleo ya viwanda na uchumi wa nchi.
“Serikali ya Awamu ya Sita imefanya jitihada za kujenga vyuo vipya vya ufundi stadi, ukarabati na upanuzi wa vyuo vya zamani pamoja na uwekaji vifaa kwa gharama ya shilingi bilioni 233.7, inafanya haya ili kuboresha na kuwasogezea wananchi fursa hasa wale wenye kipato cha chini waweze kunufaika kupata mafunzo bora na kwa gharama nafuu”, amesema CPA. Anthony.
Amefafanua kuwa, katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2024, Serikali ilikamilisha ujenzi wa vyuo 33 vya ufundi stadi ambapo 29 vikiwa vya wilaya na vinne vya mikoa kwa gharama ya Shilingi bilioni 94.5. Vilevile, Serikali ilitenga Shilingi bilioni 103 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vipya 64 vya wilaya na kimoja cha mkoa wa Songwe ambavyo vitachangia ongezeko la udahili wa wanafunzi 89,700.
Ameongeza kuwa, mpango huo pia unalenga kuongeza uwezo wa udahili katika Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi cha Morogoro kutoka wanafunzi 274 hadi wanafunzi 600 kwa kuongeza karakana za kutolea mafunzo kwa vitendo pamoja na mabweni ya wanafunzi wa kike na kiume hivyo kuwezesha kuongeza fursa za utoaji wa mafunzo ya ualimu kwa ajili ya kwenda kufundisha kwenye Shule za Sekondari za Amali na Vyuo vya VET.
Pia, Serikali imefanya upanuzi wa miundombinu ya kutolea elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini kwa kuongeza majengo mapya na ukarabati wa majengo ya zamani ili kuweka mazingira wezeshi ya kukuza ubora wa mafunzo na kuongeza fursa za udahili katika vyuo vya VETA ambapo katika kipindi cha miaka minne, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 14.2 kwa ajili ya miradi hiyo.
Fedha hizo zimewezesha uboreshaji na upanuzi wa miundombinu ya vyuo vya Newala, Ngorongoro, Moshi, Dar es Salaam (Chang’ombe), Kipawa, Mtwara, Mwanza, Mikumi, Karagwe, Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) Kihonda, Nkasi, Nyamidaho, Kanadi, Ileje, Namtumbo, Mabalanga, Gorowa, Arusha na Busokelo.
Kwa sasa VETA ina vyuo 80, mwishoni mwa mwaka 2025, vyuo vinavyojengwa vinatarajiwa kukamilika na kufanya idadi ya vyuo hivyo kufikia 145. Aidha, Serikali imefanya maboresho ya vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika vyuo vya VETA na imetoa Shilingi bilioni 22 ili mafunzo yatolewe kwa teknolojia ya kisasa.