Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kwa dhati kuondoa uzembe na vitendo vyovyote vya rushwa mahali pa kazi hii ikiwa ni pamoja na kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza tija katika utendaji wa kazi.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi wakati akifungua mkutano wa sita wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi hiyo uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam ambao ulipitia makadirio ya bajeti ya JKCI kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Prof. Janabi alisema ni wajibu wa kila mfanyakazi kuhakikisha anafahamu wajibu wake mahali pa kazi, anafanya kazi kwa bidii, anatekeleza malengo aliyopangiwa katika muda uliopangwa. Vilevile kwa mfanyakazi anatakiwa kutunza mali na vifaa alivyokabidhiwa kufanyiwa kazi na kuwahi kazini ili kuiwezesha Hospitali hiyo kusonga mbele katika kutekeleza malengo ya Serikali pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Mfanyakazi wa JKCI anatakiwa kufahamu ni huduma ya kiwango gani aitoe kwa wagonjwa na ndugu zao wakati huo huo ni lazima ajue bajeti iliyotengwa kwa ajili ya shughuli zake ndani ya Taasisi ili afanye kazi kwa kuzingatia malengo na rasilimali zilizokadiriwa kutumika”.
“Utaratibu ambao bajeti huandaliwa kulingana na mipango kazi iliyoainishwa kwenye mpango mkakati wa Taasisi kulingana na vyanzo vya mapato na rasilimali zilizopo. Mtindo huu wa bajeti huonesha wazi wazi utendaji wa kila idara hususan kwa mtu mmoja mmoja kulingana na vipimo vya utendaji wake”, alisema Prof. Janabi.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya JKCI kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Mkurugenzi wa Fedha na Utawala CPA Agnes Kuhenga alisema bajeti hiyo ya shilingi bilioni 44.6 imelenga zaidi katika ununuzi wa vifaa tiba na vitendanishi, madawa, ujenzi wa jengo la utawala na vipimo, mafunzo kwa watumishi na mishahara na posho za wafanyakazi.
Aidha CPA Agnes alisema katika kuboresha kipato cha wafanyakazi, Taasisi hiyo ilianzisha Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) mwaka 2019 ambayo hadi sasa kina wanachama 91 ambao ni wafanyakazi wa JKCI na tayari kimeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 200.
“Kuwepo kwa JKCI SACCOS kumewasaidia kwa kiasi kikubwa wafanyakazi wetu kuweka akiba na kupata mikopo ambayo wanaitumia katika shughuli za maendeleo yao binafsi ili kujikwamua kiuchumi. Jambo la kufurahisha ni kuwa wanachama hawa wanalipa mikopo yao kwa wakati na hivyo kuiwezesha SACCOS hii kuwa na mafanikio makubwa zaidi”, alisema CPA Kuhenga.
Kwa upande wake Mwenyekiti mteule wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi hiyo Prof. William Mahalu aliipongeza managenenti ya JKCI kwa kuwa na maelewano mazuri baina yao na wafanyakazi, uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE)na baraza la wafanyakazi jambo linalosaidia kuwepo na utoaji mzuri wa huduma kwa wagonjwa na wananchi wanaowahudumia.
Prof. Mahalu ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo katika Hospitali ya Kanda Bugando aliwapongeza wafanyakazi wa JKCI kwa huduma bora na za kisasa za matibabu ya moyo wanazozitoa kwa wagonjwa na kuwaomba waendelee na moyo huo huo ili huduma hizo ziwe endelevu ili wagonjwa waendelee kutibiwa hapahapa nchini na siyo nje ya nchi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Ninawapongeza kwa bajeti nzuri mliyoiandaa ambayo imegusa idara zote za Taasisi ikiwepo kutengwa kwa fedha za kuwasomesha wafanyakazi. Ninawaomba wale ambao mtapata nafasi ya kwenda kusoma muitumie vizuri nafasi hiyo ili mtakapomaliza mrudi na ujuzi ambao utaboresha utoaji wa huduma kwa wananchi”, alisema Prof. Mahalu.