Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali, Wadau Kutengeneza Mfumo Jumuishi Kuimarisha Huduma za Ustawi wa Jamii
Apr 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na WMJJWM, Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta pamoja na wadau wa Ustawi wa Jamii, ina mpango wa kutengeneza mfumo jumuishi utakaosaidia kusimamia na kupatikana kwa taarifa za huduma za ustawi wa jamii nchini.

Akifungua kikao kilichoikutanisha Wizara, Wizara za kisekta na Wadau, kwa lengo la kujadili namna ya kutengeneza mfumo huo, jijini Dodoma tarehe 14 Aprili, 2022, Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wadau kuhakikisha mfumo unaopendekezwa unakidhi mahitaji na kutatua changamoto za mifumo iliyopo.

Mhe. Dkt. Gwajima amesema Wadau pamoja na Serikali wamekuwa wakishirikiana nyakati zote kuanzisha na kuendesha mifumo ya taarifa za huduma za ustawi wa jamii lakini mifumo hiyo imekuwa ikifanyia kazi kundi moja la watoto tu na kuyacha makundi mengine,  hivyo mfumo unaopendekezwa ujumuishe Makundi yote yanayostahili kuwepo.

"Mifumo hii bado ina mapungufu, lazima tufanye kazi kwa pamoja kwani bado haijumuishi huduma zote za Ustawi wa Jamii kwa walengwa wote kama vile wazee na makundi mengine yanayohudumiwa na Ustawi wa jamii",  alisema Dkt. Gwajima

Ameongeza kuwa mifumo iliyopo (MVC- MIS na DCMS) inalenga watoto pekee hivyo kukosa taarifa muhimu kuhusu huduma zinazotolewa kwa makundi mengine. 

Aidha, Dkt.  Gwajima amebainisha kuwa mfumo Jumuishi unaopendekezwa utasaidia kupata takwimu za huduma katika vituo vya kutolea huduma kama vile makazi ya wazee, nyumba salama , vituo vya mkono kwa mkono, vituo vya kulelea watoto wadogo mchana na makao ya watoto.

"Ili kukamilisha mfumo huu pamoja na kuhakikisha unafanya kazi nchi nzima tunahitaji fedha kiasi cha Dola za Marekani 600,000 sawa na fedha za kitanzania bilioni 13.8 ", alisema Dorothy Gwajima 

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwajuma Magwiza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi,  amebainisha changamoto zilizopo katika mifumo ya awali kuwa ni pamoja na kushindwa kuendana na mahitaji tarajiwa ya Wizara na wadau kwa ujumla ikiwemo kukosa uwezo wa kufuatilia usimamizi wa shauri kwa mtoto mmoja mmoja, hali inayozuia Wizara pamoja na wadau kutumia mfumo huo kutengeneza afua zinazomlenga mnufaika.

"Serikali imeona ipo haja ya kutengeneza mfumo mmoja utakaojumuisha huduma zote za Ustawi wa Jamii ili kurahisisha upatikanaji wa takwimu na taarifa za huduma zinazotolewa", alisema Bi. Magwiza.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afyabna Ustawi wa Jamii Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Amina Mfaki alisema Serikali kupitia ofisi hiyo, kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali kukabiliana na tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi pamoja na huduma za msaada wa kisaikolojia kwa wahanga wa ukatili.

Bi. Amina ametaja baadhi ya shughuli zilizofanywa ni pamoja na kutoa mafunzo ya kutumia mifumo iliyopo kwa Maafisa Ustawi wa Jamii 184 katika Halmashauri zote nchini ya kupitia ushirikiano na wadau.

Akizungumza kwa niaba ya wadau walioshiriki kikao hicho, Mtaalam wa Ulinzi wa Mtoto kutoka Shirika la UNICEF, Evance Mori alisema wadau wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma kwenye maeneo mbalimbali hususani eneo hilo la taarifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi