Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuwajengea Umahiri Walimu na Wanafunzi Kupitia Mkakati wa KKK
Jan 29, 2026
Serikali Kuwajengea Umahiri Walimu na Wanafunzi Kupitia Mkakati wa KKK
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa Darasa la Kwanza na la Pili.
Na Bupe Mwaiseje - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imejipanga kuwapatia walimu na wanafunzi nyenzo pamoja na mafunzo bora ili kuwaongezea walimu ujuzi na umahiri katika ufuatiliaji wa elimu ya watoto katika hatua za awali za kujifunza.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa watoto wa elimu ya awali na wanafunzi wa Darasa la Kwanza na la Pili, leo, Januari 29, 2026, jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema Serikali inalenga kuboresha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji kupitia mbinu za kisasa.

“Tunakwenda kuwafundisha walimu na kuongeza ujuzi wao, lakini pia kuwapatia nyenzo zote zinazohitajika pamoja na mbinu za kisasa za ufundishaji na ufuatiliaji wa karibu,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa Serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa kila mtoto anayefika darasa la tatu anakuwa na uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu huku akisisitiza kuwa suala hilo sio la hiyari bali ni wajibu wa pamoja wa Serikali, wazazi na jamii kwa ujumla.

Rais Samia amesema uwekezaji katika stadi za awali za mafunzo ni msingi muhimu wa kuimarisha sekta ya elimu nchini na kujenga rasilimali watu yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu nchini, ambapo idadi ya madarasa ya shule za msingi imeongezeka kutoka 151,315 mwaka 2021 hadi 184,550 mwaka 2025 na kwa upande wa shule za sekondari imeongezeka kutoka 64,204 mwaka 2021 hadi 101,473 mwaka 2025.

Kuhusu ajira za walimu Rais Samia amesema zimeongezeka na tayari walimu 6,044 wameajiriwa huku walimu 956 wakiwa katika hatua za mwisho za mchakato wa ajira, ambao unatarajiwa kukamilika Februari 3 mwaka huu.

Aidha, ameeleza kuwa Saerikali kupitia Wizara ya Elimu itaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wa elimu katika kuwapatia walimu nyenzo na mafunzo, ili kuhakikisha mpango mkakati wa KKK unatekelezwa kikamilifu katika ngazi zote na kuleta matokeo chanya kwa vitendo

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi