Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kutumia Trilioni 1.2 Kuijenga Upya MNH
Mar 06, 2025
Serikali Kutumia Trilioni 1.2 Kuijenga Upya MNH
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Rachel Mhaville akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi, kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Taasisi hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita tarehe 6 Machi, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Sita kwa kushirikiana na Serikali ya Korea, zinaendelea na hatua mbalimbali za kusaini mkataba kwa ajili ya mradi wa kujenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa gharama ya shilingi Trilioni 1.2 ambapo kati ya hizo, Serikali ya Tanzania itachangia USD. Milioni 104 na Serikali ya Korea Kusini itachangia dola za Marekani Milioni 364.

Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Rachel Mhaville ameyasema hayo,  leo Machi 06, 2025 katika ukumbi wa Idara ya Habari- MAELEZO jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Hospitali hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ikiwa ni programu iliyoandaliwa na Idara hiyo.

“Hospitali ya Taifa Muhimbili itaboreshwa kwa kujengwa upya ili kuwezesha huduma zote kutolewa ndani ya jengo moja litakalokuwa na vitanda 1,757 kutoka 1,435 vya sasa ambapo upembuzi yakinifu wa mradi huu umekamilika na utekelezaji wa mradi huu ni wa awamu moja ambao kukamilika kwake kutachukua miaka mitano baada ya kusaini mkataba”, amesema Dkt. Rachel Mhaville.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi huo wa kihistoria katika sekta ya afya nchini utakuwa na faida lukuki ikiwemo kuboreshwa kwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kupitia vifaa tiba vya kisasa ambapo Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya fedha kusafirisha wagonjwa nje ya nchi.

Vile vile, itawezesha wagonjwa kupata huduma zote katika eneo moja, kupunguza mizunguko na usumbufu pamoja na kuwa mpangilio mpya wa hospitali huku eneo kubwa likibaki wazi, kwa matumizi ya maendeleo mengine miaka 50 ijayo.

Hospitali ya Taifa Muhimbili yenye kampasi mbili, ni Hospitali ya Rufaa ya Kitaifa na kubwa kuliko zote nchini yenye vitanda 2,043 ambapo katika eneo la Upanga kuna vitanda 1,435 na eneo la Mloganzila vipo 608.

Katika Kampasi zote mbili, wagonjwa 4,000 wanaonwa kwa siku ambapo Upanga jumla ya wagonjwa 2,700 wanahudumiwa ikiwa ni wagonjwa wa nje 1,700 na wagonjwa waliolazwa wodini wakati wote ni 1,000.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi