Serikali imepanga kutoa jumla ya ajira 52,124 katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha utendaji kazi katika sekta mbalimbali na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi hiyo bungeni jijini Dodoma.

Amesema kati ya ajira hizo, nafasi 45,000 zitakuwa ajira mpya zitakazojazwa katika taasisi za umma kulingana na ikama zilizoidhinishwa, huku nafasi 7,124 zikiwa ni za ajira mbadala kwa kada mbalimbali.
“Katika mwaka 2026/27, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma imepanga kushughulikia vibali vya ajira mpya na mbadala ili kukidhi mahitaji ya watumishi katika taasisi za umma,” amesema Mhe. Kikwete.

Aidha, ameeleza kuwa ofisi hiyo itahakiki na kuidhinisha madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi katika taasisi 425, pamoja na kushughulikia maombi ya malimbikizo kwa wafanyakazi waliokoma utumishi kutoka kwa waajiri 200.
Katika hatua nyingine, Serikali itaendelea kusafisha na kuhakiki taarifa za watumishi katika taasisi 127 zinazotumia mfumo wa e-Watumishi, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwazi na ufanisi katika utumishi wa umma.

Pia, huduma zitaendelea kutolewa kwa viongozi wa kitaifa wastaafu 21, wakiwemo viongozi 10 na wajane 11, kwa mujibu wa sheria.