Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba amesema ipo haja kutafuta namna ya kuboresha upatikanaji wa fedha za kigeni nchini Tanzania kwa maslahi ya Uchumi wa nchi.
Haya ameyasema Julai 17, 2023 jijini Dar es salaam wakati akifungua kikao cha ndani cha wamiliki wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni pamoja na wanaofanya biashara hiyo kujadili namna bora ya kufanya maboresho katika mzunguko wa fedha za kigeni hapa nchini.
Bw. Tutuba amesema maboresho hayo ni muhimu kufanyika ili kuufanya mfumo uweze kuleta ufanisi katika kuzifanya fedha za kigeni zionekane katika mfumo zinapoingia au kutumika na wageni hapa nchini.
Aidha, Bw. Tutuba amezitaja baadhi ya sababu zilizochangia kuleta upungufu wa Fedha za kigeni kuwa ni pamoja na mlipuko wa Ugonjwa wa Corona, vita vya Urusi na Ukraine, na mabadiliko ya tabianchi.
“Tunatambua uhaba wa fedha za kigeni chanzo ni kama vile corona na vita vya Urusi na kule Ukraine, ambapo watu walipotoka Lock down walihitaji zaidi fedha za kigeni kuliko kawaida,” alisema Bw. Tutuba.
Hatahivyo, Bw. Tutuba alisema Uchumi wa Tanzania umekua kwa asilimia 4.7 kufuatia jitihada za Uongozi wa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mikakati ya kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kutumika kununua bidhaa nje.
Akisisitiza Gavana Tutuba aliongeza kuwa uzalishaji wa bidhaa zenye kiwango kwa ajili ya kuuza nje umeimarishwa ili kupata fedha za kigeni.
Aliwasihi wadau hao wa fedha za kigeni kuwa lengo la kuwaita leo ni kutaka kuwasikiliza na kujadiliana nao ili kuona namna gani kila mmoja anapata faida na kodi inalipa ipasavyo.