[caption id="attachment_3978" align="aligncenter" width="300"] Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Wambali. (Picha na: Maktaba)[/caption]
Na. Tiganya Vincent-RS TABORA
Mahakama ya Tanzania imesema itaendelea kuziboresha Mahakama za Mwanzo na kujenga mpya katika kila kata ili kusogeza huduma za usikilizaji wa mashauri mbalimbali karibu na wananchi na hivyo kuwafanya kuendelea na shughuli za kimaendeleo badala ya kutumia muda mwingi kufuata huduma za kimahakama.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Tabora na Jaji Kiongozi Mhe. Ferdinand Wambali wakati wa ziara ya kikazi katika mikoa ya Tabora na Kigoma, kwa ajili ya kukagua shughuli za usikilizaji wa mashauri mbalimbali kama walivyojiwekea malengo ya kuharakisha usikilizwaji wa mashauri.
Jaji Kiongozi alisema kuwa kuna Wilaya zinategemea Mahakama za maeneo mengine na nyingine kama vile Sikonge ina Mahakama moja tu, jambo ambalo linawafanya wakazi wake kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za Kimahakama katika Wilaya ya Tabora.
Alisema kuwa Mahakama ya Tanzania itaendelea kuboresha Mahakama za Mwanzo zilizopo na kujenga mpya katika maeneo yote ambayo hayana huduma hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma hizo karibu na wanapoishi hivyo kutumia muda mfupi kufuatilia mashauri na uliobaki katika shughuli nyingine za kiuchumi.
Jaji Kiongozi huyo aliongeza kuwa lengo ni kuhakikisha kuwa kila shauri linalofika katika Mahakama ya Mwanzo lisizidi miezi sita na lile linakwenda katika Mahakama za Wilaya na zile za Hakimu Mkazi lisizidi mwaka mmoja wakati Mahakama Kuu lisizidi miaka miwili.
Alitoa wito kwa Mamlaka zinazohusika na utoaji wa ardhi kutoa kipaumbele pindi Mahakama inapohitaji eneo la ujenzi majengo ya Mahakama ili kazi ifanyike kwa wakati na hivyo wananchi waweze kusafiri umbali mfupi kufuata huduma za kutafuta haki yao.
Jaji Kiongozi alisisitiza kuwa ucheleweshaji unaoweza kufanyika wakati wao wanahitaji eneo la ujenzi linawaathiri pia wananchi wanaokuwa wakihitaji huduma hiyo kwa karibu zaidi.
Katika hatua nyingine, Jaji Kiongozi Wambali alisema kuwa Mahakama ipo katika mpango wa kuhakikisha Mashauri yaliyochukua muda mrefu yanamalizika haraka ili kutoa fursa kwa wahusika kuendelea na shughuli nyingine za kiuchumi badala ya kuendelea na kesi.
Alisema kuwa hatua hiyo ni pamoja na kuboresha miundo mbinu ya Mahakama ili iweze kurahisisha utendaji wa shughuli za chombo hicho.