[caption id="attachment_33421" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Juani, Kata ya Jibondo, Wilaya ya Mafia, alipokuwa katika ziara ya kazi Kisiwani humo, mwishoni mwa Juma, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.[/caption]
Na Veronica Simba – Mafia
Serikali kupitia Wizara ya Nishati, imeandaa mkakati wa kupeleka umeme katika Visiwa vyote nchini kwa kutumia nishati mbadala, hususan umeme jua.
Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, mwishoni mwa Juma wakati wa ziara yake kisiwani Mafia, kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme na kuzungumza na wananchi.
Akizungumza na wananchi wa Mafia kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali, Naibu Waziri aliwahakikishia kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kupeleka umeme wa kutosha na wa uhakika katika Visiwa vyote ili kutekeleza kwa vitendo azma ya kuwezesha uchumi wa viwanda.
“Maeneo ya Visiwa tutayasimamia zaidi kwa sababu ya umaalum wake. Ndiyo sababu hata nishati tutakayoileta ni maalum,” alisema.
Akifafanua zaidi, Naibu Waziri alisema kuwa, zoezi husika litaanza mwezi Septemba mwaka huu, kwa kuzipelekea Taasisi zote za Umma visiwani zikiwemo Shule, Hospitali na nyinginezo, Paneli za Umeme Jua ili kuboresha utoaji wa huduma katika sehemu hizo.
[caption id="attachment_33422" align="aligncenter" width="890"] Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mbele) na Ujumbe wake wakiwasili katika Kijiji cha Juani, Kata ya Jibondo, Wilaya ya Mafia, mwishoni mwa Juma, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme na kuzungumza na wananchi.[/caption]Awali, akizungumza katika mkutano huo wa Naibu Waziri, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Hussein Shamdas alisema kuwa, Utafiti kuhusu Mradi huo wa kuzipelekea Taasisi za Umma Paneli za umeme jua, ulishafanyika na kukamilika. “Ndiyo maana mwezi wa Tisa, tutaanza kusambaza Paneli hizo.”
Kuhusu Mradi mkubwa wa kuwaunganishia wananchi huduma ya umeme unaotumia nguvu ya jua, Shamdas alieleza kuwa, kazi inayofanyika kwa sasa ni kutafuta eneo itakapofungwa mitambo mikubwa ya umeme jua, ambayo ndiyo itakayotumika kuwasambazia nishati hiyo pindi zoezi la kuifunga litakapokamilika.
Akifafanua zaidi, alisema kuwa, umeme utakaofungwa utakuwa na nguvu sawa na ule uliozoeleka, unaotokana na nguvu ya maji au dizeli. “Msije mkafikiria ni hivi vi-sola vidogo vidogo, la hasha. Ni umeme mkubwa na utawaleteeni maendeleo.”
Naibu Waziri aliwapongeza wananchi wa Mafia kwa mwamko waliouonesha katika kuhitaji umeme. Aliwataka kufanya maandalizi ya kutosha, ili waweze kuutumia umeme utakaopelekwa ipasavyo katika kuinua uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.
[caption id="attachment_33423" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili kutoka kushoto), akiwaeleza baadhi ya wafanyakazi wa Zahanati ya Marimbani iliyoko wilayani Mafia (kulia), namna ya kutumia Taa za Umeme Jua, kabla ya kuwakabidhi Seti mbili za Taa hizo ili zisaidie kuboresha utoaji huduma. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi wilayani Mafia, mwishoni mwa Juma.[/caption]Kwa upande wao, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaibu Nnunduma na Mbunge wa Jimbo hilo, Mbaraka Dau, waliwaasa wananchi wa Kisiwa hicho, kuachana na utamaduni wa kudai fidia kwa mazao mbalimbali yatakayoondolewa ili kuruhusu kupitisha miundombinu ya Mradi husika.
Aidha, waliwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha wakati Mradi huo utakapoanza kutekelezwa kwani ni wenye manufaa kwao.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alikabidhi Seti mbili za Vifaa vya Taa zinazotumia umeme wa jua kwa kila Zahanati za Vijiji alivyotembelea wilayani humo kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma.
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) iliyotolewa kwa Naibu Waziri na Meneja wa Wilaya husika, Patience Ndunguru; Wilaya hiyo inazalisha umeme kwa kutumia mitambo ya dizeli tangu mwaka 1970. Umeme unaozalishwa hautoshelezi mahitaji kutokana na changamoto mbalimbali, jambo lililosababisha Serikali kutafuta mbinu mbadala ya kupeleka umeme mwingi zaidi na wa uhakika.