Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kupanda Miti Bilioni 1 Mlima Kilimanjaro
Feb 04, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na. Immaculate Makilika

Serikali imeandaa programu mbalimbali za kutunza mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti zaidi ya bilioni moja katika eneo la Mlima Kilimanjaro ili kukabiliana na matatizo ya mabadiliko ya tabia nchi.

Akijibu swali leo Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Zungu alisema,“Programu ya kwanza ni kupanda miti zaidi ya bilioni moja katika eneo la Mlima Kilimanjaro ili kulinda barafu iliyopo  katika nchi yetu, pamoja na kuanza mkakati wa  kuomba fedha zilizopo katika Mfuko  mpya  ulioanzishwa na nchi ya Ufaransa, wa dola za kimarekani  bilioni 100, ulioanzishwa kwa lengo la kuboresha mazingira katika nchi zenye uhitaji, ikiwemo Tanzania”.

Aidha, Waziri Zungu aliongeza kuwa mkakati huo wa kupanda miti na kuitunza hivi sasa unaandaliwa katika wilaya zote nchini, na miti itakayopandwa katika kila wilaya itakuwa ya aina maalumu ili kuendana na mazingira yaliyopo katika wilaya husika.

“Nchi yetu imebarikiwa kuwa na asilimia 39.9 ya  misitu, misitu hii inapotea, kuanzia mwaka  1990 hadi mwaka 2010 tumeshapoteza takribani  ekari  milioni 8 ya misitu, na hii ni hatari kubwa sana kwa watanzania,  tuhakikishe  tunaacha kukata miti,  tutumie  miti kama fursa ya kibiashara, badala ya kuikata tuweke mazao ya nyuki”,  amesisitiza Waziri Zungu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi