Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kukuza Sekta ya Uwekezaji Nchini
Apr 06, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Miradi ya Wawekezaji 294 imesajiliwa

Na Georgina Misama – MAELEZO, Dar es Salaam

Serikali imesema hadi kufikia Februari, 2022 imefanikiwa kuvutia wawekezaji katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kusajili jumla ya miradi ya uwekezaji 294.

Akizungumza leo April 06, 2022, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati akiwasilisha Hotuba ya Makadirio na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2022/23 Bungeni Jijini Dodoma, alisema thamani ya miradi iliyosajiliwa ni Dola za Kimarekani bilioni 8.04.

“Hadi kufikia Februari, 2022 Serikali imefanikiwa kuvutia uwekezaji na kusajili jumla ya miradi ya uwekezaji 294 yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 8.04 ambazo sawa na shilingi trilioni 18.58 ikilinganishwa na dola za Kimarekani bilioni1 mwaka 2020/2021,” alisema Mhe. Majaliwa.

Maeneo mengine aliyoyaongelea ni pamoja na sekta ya elimu ambapo alisema Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa kuongeza fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi ambapo katika mwaka 2021/2022, jumla ya shilingi bilioni 570 zimetumika ikilinganishwa na shilingi bilioni 464 zilizotumika mwaka 2020/2021.

Tumeendelea kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ambapo katika mwaka 2021/2022, Serikali imekamilisha ujenzi na ukarabati wa vyuo 14 vya Maendeleo ya Wananchi na ujenzi wa vyuo vipya 25 vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) vya wilaya,” aliongeza.

Kwa upande wa sekta ya Utalii, Mhe. Waziri Mkuu alisema kwamba utalii wa ndani umeendelea kuimarika ambapo idadi ya watalii wa ndani waliotembelea maeneo ya hifadhi iliongezeka kutoka 562,549 mwaka 2020 hadi kufikia zaidi ya laki 7 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 40.2.

Utekelezaji wa mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere wenye MW 2,115 umefikia 56.79% ambapo ujenzi wa handaki la kuchepushia maji umekamilika hivi sasa ujenzi wa kituo cha kupokea na kusafirisha umeme, njia ya kupitisha maji ya kufua umeme, nyumba ya mitambo ya kufua umeme, ujenzi wa tuta kubwa la bwawa na utengenezaji wa mitambo tisa ya kuzalisha umeme.

Aidha, Serikali imefanikiwa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na nchi ya Msumbiji kutokea eneo la Mangaka hadi Mtambaswala. Hatua hii imefanya nchi zilizounganishwa na Mkongo wa Taifa kufikia saba.

Vilevile amesema kuwa, Serikali itahakikisha nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inaunganishwa kupitia Ziwa Tanganyika na hivyo kufanya nchi yetu kuwa kitovu cha mawasiliano katika ukanda wa maziwa makuu kuelekea uchumi wa kidijitali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi