Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kukamilisha Miradi Yote ya Chato - Rais Samia
Mar 17, 2022
Na Jacquiline Mrisho


Na Lilian Lundo - MAELEZO 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, miradi yote iliyopangwa na iliyoanza kutekelezwa wilayani Chato itakamilika. 

Rais Samia amesema hayo leo Machi 17, 2022 Chato, mkoani Geita wakati wa kumbukizi ya mwaka mmoja wa kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. 

"Kwa hapa Chato nataka niwahakikishie kwamba miradi yote  tuliyopanga na ambayo tumeshaanza kutekeleza tutaikamilisha hata ile midogo midogo," alisema Rais Samia. 

Aliendelea kusema kuwa, anafahamu juu ya ujenzi wa kivuko cha "Hapa Kazi Tu" kinachofanya kazi kati ya Chato na Nkome ambacho kimekamilika kwa asilimia 100 na kimegharimu shilingi bilioni 3.1.

 Vilevile, ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Chato, ambao umefikia asilimia 95 kwa gharama ya shilingi bilioni 58.9 na stendi mpya ya Chato ambayo imegharimu shilingi bilioni 13.2 ambayo imefikia asilimia 90, na mabasi madogo yameshaanza kuingia. 

Rais Samia amesema, amearifiwa kuwa ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda inayojengwa kwa shilingi bilioni 34 unaendelea vizuri na baadhi ya huduma zimeanza kutolewa. 

"Nataka niwaahidi Wanachato, miradi hii itakapokamilika kabisa, nitakuja mwenyewe kuifungua kama ambavyo angefanya Dkt. Magufuli kama angekuwepo" alisisitiza Rais Samia. 


Pia alisema kuwa, Serikali imeendelea  kuboresha na kuendeleza huduma za jamii ikiwemo afya, maji, elimu na umeme kama inavyoelekezwa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kama walivyojipanga kutekeleza. 

"Mtakumbuka katika hotuba yangu ya mwanzo kabisa baada ya kuapishwa nilisisitiza kwamba nitayaendeleza mema yote aliyotuachia Hayati Magufuli na kuleta mema mengine mapya," alisema Rais Samia. 


Aidha amesema kuwa, wanataka kujenga Tanzania ya kisasa na kuboresha maisha ya Watanzania wote na haya yote  yatafanikiwa ikiwa umoja, amani na mshikamano wetu Watanzania utadumishwa. 

Rais Samia amewashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuliombea Taifa na kuliweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu.


Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi