Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kujenga Daraja Mto Malagarasi
Jul 09, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Serikali imesema inatarajia kujenga daraja la kudumu katika mto Malagarasi litakalounganisha kijiji cha Ilagala na Kajeje ikiwa ni mbadala wa kivuko cha Malagarasi ili kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji katika maeneo hayo.


Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo wilayani Uvinza, mkoani Kigoma, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema kuwa  Serikali imeona adha wanayoipata wananchi wa hapo, hivyo imeamua ndani ya mwaka huu  wa fedha kuanza mchakato wa ujenzi wa daraja hilo.


"Sisi kama Serikali tumeona changamoto zenu hapa, hivyo tayari tumetenga kiasi cha shilingi milioni 400 ndani ya mwaka huu wa fedha 2021/2022, kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja hili, baada ya kazi hii kufanyika, ujenzi utaanza mara moja, amesema Kasekenya.

Aidha, Naibu Waziri amemuagiza Kaimu Meneja wa Kivuko hicho kuhakikisha anaongeza muda wa utoaji huduma za usafirishaji unaotolewa Kivukoni hapo hususan katika kipindi cha kiangazi, kutoka  saa 12  asubuhi hadi saa 12 usiku kama ilivyokuwa awali na kusogezwa hadi saa Tatu usiku ili kuruhusu unafuu na urahisi kwa watumiaji wa huduma hiyo huku wakisubiri ujenzi wa daraja hilo kuanza.


Halikadhalika, Kasekenya, amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Japhet Maselle, kuhakikisha anawalipa mishahara yao ya miezi nane wafanyakazi wa Kampuni ya ulinzi ya M.M Security inayofanya shughuli za ulinzi katika kivuko hicho ndani ya mwezi huu.


Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kasekenya, amekagua barabara ya Simbo- Ilagala- Kalya (Km 231.29), ambapo  amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo utaenda sambamba na uboreshaji wa barabara hiyo kutokana na umuhimu wake wa kusafirisha mazao mkoani Kigoma na nchi jirani za  Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwani tayari ipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapunduzi na pia ishaingizwa katika mpango wa utekelezaji.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara ( TANROADS), mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, amesema kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina utafanyika mapema katika mwaka huu wa fedha   ambapo kwa sasa TANROADS ipo katika mchakato wa kutangaza kazi hiyo ili kupata mhandisi mshauri kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.


Naye, Kaimu Meneja wa Kivuko cha Mv. Malagarasi, Mhandisi Halfan Juma, amesema kuwa ujio wa daraja katika maeneo hayo kutafungua fursa za kibiashara na uchumi katika wilaya hiyo na mkoa kwa ujumla.

Awali, mwananchi wa kijiji cha Kajeje wilayani hapo Bi. Ningejua Juma, ameeleza kuwa wajawazito hujifungulia njiani na wengine hupoteza maisha kutokana na abiria kusubiri muda mrefu kupata huduma ya kivuko hicho na pia kukosa huduma wakati wa usiku.


Naibu Waziri Kasekenya yupo katika ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Kigoma ambapo pamoja na mambo mengine amekagua barabara ya Simbo- Ilagala- Kalya (Km 231.29) pamoja na Kivuko cha Mv. Malagarasi. 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi