Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuja na Mfumo wa Uratibu wa Afua za Vijana
Aug 04, 2023
Serikali Kuja na Mfumo wa Uratibu wa Afua za Vijana
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi akizungumza na vijana pamoja na wadau wa Asasi za Kiraia zinazojishughulisha na masuala ya vijana katika kongamano la vijana lililofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.
Na Adam Haule

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi amesema Serikali inaandaa Mfumo wa Taifa wa Uratibu na Tathmini wa Afua za Masuala ya Maendeleo ya Vijana Nchini utakaosaidia kuwatambua na kuwaratibu wadau.

Kutokana na hilo, amemuagiza Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo na Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuzifanyia tathmini Asasi za Kiraia zinazoshughulikia masuala ya vijana ili kujua utendaji kazi wake na kama zinakidhi tija kwa vijana.

Sehemu ya vijana wakifuatilia kwa makini hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa kongamano la vijana lililofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.  

Mhe. Katambi ameyasema hayo Agosti 3, 2023 kwenye uzinduzi wa kongamano la vijana lililoandaliwa na Asasi za Kiraia 32 zinazojishughulisha na masuala ya vijana.

“Niwaagize Katibu Mkuu na Msajili wa mashirika haya mfanye tathmini ili kuhakikisha asasi hizi zinatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na malengo ya serikali ili kuleta tija kwa vijana nchini,”amesema Katambi.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Maendeleo ya Vijana mkoani Dodoma (DOYODO), Rajab Juma ameomba serikali kuzitengea ruzuku asasi zinazojihusisha na masuala ya vijana kama ilivyo kwa Vyama vya Siasa ili kulifikia kundi kubwa la vijana katika kujenga kesho yao.

Baadhi ya Viongozi na Wadau wa Asasi za Kiraia zinazojishughulisha na masuala ya vijana katika kongamano la vijana wakifuatilia mada mbalimbali katika kongamano hilo. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Idara ya Demokrasia, Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bret Saalwaechter ameipongeza serikali kwa ushirikishwaji wa vijana, wanawake na Watu Wenye Ulemavu katika kuwaletea maendeleo na kushughulikia changamoto zao.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Freedom House, Daniel Lema, amesema bado kuna kundi la vijana wanashindwa kutumia fursa zinazowazunguka ili kutengeneza kipato na kuishia kulalamika.

Kongamano hilo limeongozwa na Kauli mbiu isemayo “Ushiriki wa Vijana kwenye Uongozi na Utawala Bora kwa Maendeleo ya kiuchumi”.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi