Na Georgina Misama – MAELEZO
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imependekeza kufuta ada kwa wanafunzi wanaochaguliwa kuendelea na masomo kwa shule za Sekondari za Serikali kwa kidato cha tano na sita.
Akitoa pendekezo hilo, Bungeni Jijini Dodoma Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba alisema hakuna shule za Kata zenye kitado cha Tato na Sita na hivyo watoto wanaofaulu wanapata adha ya kwenda mbali, wakati akiwasilisha mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
“ Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anaguswa sana na tatizo la ukosefu wa shule za kata za kidato cha tano na sita jambo linalowalazimu wanafunzi wanaochaguliwa kuendelea na masomo kwenda shule za mbali na kupelekea kuongezeka kwa gharama, napendekeza kufuta ada ya kidato cha tano na sita ili kuwapunguzia wazazi na wanafunzi hao mzigo wa gharama hizo,” aliongea Dk. Mchemba.
Alisema kwa sasa idadi ya wanafunzi wa kidato cha tano ni takribani 90,825 na kidato cha sita ni 56,880 ambapo kwa ujumla wao wanahitaji kiasi cha shilingi bilioni 10.3, ili kukidhi mahitaji yao ya kieleimu.
Uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Sita kufuta ada utakaporidhiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utaifanya Tanzania kuwa nchi inayotoa elimu bure kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha sita.