Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kufanya Utafiti Mji wa Tunduma Kubaini Fursa za Kukuza Uchumi
Feb 02, 2024
Serikali Kufanya Utafiti Mji wa Tunduma Kubaini Fursa za Kukuza Uchumi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalaum, Mhe.  Neema Mwandabila leo Februari 2, 2024 bungeni jijini Dodoma.
Na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji

Serikali imesema kuwa Tume ya Mipango itafanya tafiti mbalimbali kubaini fursa za maendeleo katika miji ikiwemo Mji wa Tunduma kwa lengo kujua ni jinsi gani mji huo na miji mingine inaweza kuongeza kasi ya maendeleo na kuchangia kukuza uchumi wa nchi.

 

Hayo yameelezwa leo Februari 2, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalaum, Mhe.  Neema Mwandabila, aliyeuliza kuhusu mkakati wa Serikali wa kufanya utafiti maalum katika Mji wa Tunduma ili kubaini ni namna gani unaweza kuchangia kukuza uchumi wa nchi.

 

“Tume ya Mipango imejipanga kufanya tafiti mbalimbali na kuratibu tafiti zitakazofanywa na taasisi nyingine za umma na binafsi kwa lengo la kubaini fursa za maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Mipango, hususani kifungu cha 6(2), pamoja na majukumu mengine, Tume ya Mipango ina jukumu la kufanya utafiti kuhusu suala lolote ambalo Tume inaona ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa”, ameeleza Prof. Mkumbo.

 

Vilevile, Prof. Mkumbo amejibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mhe. Angelina Mabula kuhusu utekelezaji wa mradi wa kongani la viwanda lenye ekari 52 lilotengwa katika Manispaa ya Ilemela eneo la Nyamanoro.

 

Ambapo, Prof. Mkumbo amesema “Eneo hilo limeshakabidhiwa katika Taasisi ya EPZA na linafanyiwa kazi, aidha litawasilishwa katika Bodi na baada ya hapo litatolewa maelekezo maalumu ni  lini hasa ratiba itatoka ya utekelezaji na katika Bunge lijalo tutaeleza Mpango maalumu kuhusu kongano hilo”.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi