Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kuendelea Kuimarisha Upatikanaji wa Maji Safi na Salama Nchini
Apr 03, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_41650" align="aligncenter" width="963"] Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Hassan Suluhu akihutubia wananchi wa Songwe walioshiriki kwa wingi katika uwanja wa Kimondo – Forest, Wilayani Mbozi kushuhudia uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa Mwaka 2019.[/caption]

Na; OWM (KVAU) - Songwe

Serikali imedhamiria kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi waishio mijini kufikia asilimia 95 na vijijini asilimia 85 ifikapo 2020.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Hassan Suluhu wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Aprili 2, 2019 zilizofanyika uwanja wa Kimondo – Forest Mlowo, Wilaya ya Mbozi, Mkoani Songwe.

Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu 2019 isemayo “Maji ni Haki ya kila Mtu, Tutunze Vyanzo Vyake na Tukumbuke Kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa”

Makamu wa Rais amesema kuwa dhamira ya Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ni  kuboresha huduma za jamii ikiwemo sekta ya elimu, afya, barabara,  umeme vijijini, usafiri wa anga, uvuvi, kilimo, viwanda na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wote.

[caption id="attachment_41649" align="aligncenter" width="1000"] Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa Mkoa wa Songwe waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.[/caption]

“Sera yetu ya Maji ya mwaka 2002 inasisitiza upatikanaji wa maji safi na salama ambayo ni muhimu kwa maisha ya kila mtu, shughuli za kiuchumi na ustawi wa mazingira,” alisema Makamu wa Rais.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa maji safi, alieleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji nchini ikiwemo mabwawa ya kimkakati na kuboresha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji maji safi.

Aidha, Makamu wa Rais alitoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji kwa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kando ya vyanzo hivyo.

[caption id="attachment_41648" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Songwe walioshiriki kwenye hafla ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2019.[/caption]

Kupitia hadhara ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Makamu wa Rais, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao ni muhimu katika kuleta maendeleo ya watu na huduma za kijamii.

Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ndio msingi mkubwa wa amani, Mshikamano, Uzalendo na Umoja tulionao katika Taifa.

“Tunu hii imekuwa ni kichocheo cha maendeleo kwa wananchi na wamekuwa wakihamasika kushiriki katika kuandaa na kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo ya kijamii na kiuchumi iliyopo katika maeneo yao,” alisema Mhagama.

[caption id="attachment_41646" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Serikali ya Zanzibar, Mhe. Balozi Ali Karume akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye Uwanja wa Kimondo, Wilayani Mbozi Aprili 2, 2019.[/caption]

Waziri Mhagama aliongeza kwa kuwashukuru wadau mbalimbali waliosaidia kufanikisha tukio hilo muhimu la Kitaifa.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali (Mst.), Nicodemus Mwangela aliishukuru Serikali kwa kuchagua Mkoa wa Songwe kuwa wenyeji wa Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2019.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi