Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali kuendelea kuboresha sekta ya mawasiliano-Makamu wa Rais
Jul 11, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na. Mwandishi Wetu

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kusimamia na kuweka mazingira bora yatakayosaidia wananchi nchini kupata huduma za mawasiliano ya simu kwa njia ya kisasa zaidi Mjini na Vijijini.

Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati anafungua Mkutano wa mwaka wa Chama cha Makampuni ya Simu Duniani (GSMA MOBILE 360).

Amesema ni imani yake kuwa wadau hao wa makampuni ya simu watajadili kwa kina namna bora ya kufikisha mawasiliano ya kisasa na kuweka mipango mizuri ya kufikia wananchi wengi zaidi hasa maeneo vijijini ambayo baadhi yao hayafikiki kutokana na uduni wa miundombinu.

“Ningependa kusema kwamba Tanzania inakubali sana ushirikiano na GSMA na tunatamani kupanua ushirikiano wetu na uwezeshaji kwa watu wetu kwa njia ya mawasiliano ya simu ili kufikia utekelezaji wa ajenda za maendeleo endelevu ya Umoja wa Afrika (AU) na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2020”, amesisitiza Makamu wa Rais.

Ameleeza kuwa kwa sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi kadhaa Kusini mwa Bara la Afrika ambayo inafanya vizuri kwa wananchi wake kutuma fedha kwa kutumia simu za mkononi na kusema kuwa hilo ni jambo zuri hasa kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa na akaunti za benki, hivyo huduma hiyo huwasaidia kwa kiasi kikubwa kutuma fedha kwa urahisi.

Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa zaidi kwa huduma za kisasa za kimtandao ili wananchi waweze kunufaika zaidi kwa njia hiyo katika sekta za elimu, afya, kilimo, biashara na masuala ya kijinsia.

Amewahakikishia wadau hao kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kushirikiana nao bega kwa bega ili kuhakikisha sekta ya mawasiliano inaimarisha huduma zake kwa wananchi.

Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kujifunza kutoka nchi zingine ambazo zimefanya vizuri katika sekta ya mawasiliano ili taifa na wananchi wake waweze kunufaika ipasavyo na huduma hizo kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa ameeleza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Makampuni ya Mawasiliano ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa na ubora unaotakiwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi