Serikali kupitia Chuo cha Taifa cha Usafirishahi (NIT) kimejipanga kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Taaluma ya Usafiri wa Anga na Oparesheni ya Usafirishaji ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda katika Afrika Mashariki ujulikanao kama “East Africa Skills for Transformation and Regional Integration Project (EASTRIP)”.
Mkuu wa Chuo cha NIT, Mhandisi, Dkt. Prosper Mgaya amesema hayo wakati akieleza mafanikio na mwelekeo wa chuo hicho ndani ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Machi 20, 2025 katika ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
“NIT itapokea Dola za Marekani 21,250,000 sawa na shillingi za Kitanzania Bilioni 49 kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji, katika mwelekeo wa chuo chetu, tutahakikisha Kituo hiki kinapata ithibati za kimataifa ambazo zitakiwezesha kutoa mafunzo au mitihani kwa niaba ya Mamlaka za Usafiri wa Anga”, amesema Mhandisi Mgaya.
Ameongeza kuwa kupitia mradi huo, Serikali imekiwezesha Chuo kujenga majengo matano katika Kampasi ya Mabibo -Dar es salaam ambao ujenzi wake umefikia asilimia 97. Majengo matatu ya Kituo cha Umahiri kitakachojengwa yatakuwa na madarasa, maabara, karakana na ofisi za watumishi na majengo mawili ni mabweni ya wanafunzi yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 1,504.
Ujenzi huo unaogharimu shilingi bilioni 24.9, utakamilika ifikapo mwezi Juni 2025. Aidha, mradi huo umefadhili ujenzi wa jengo la mafunzo ya urubani katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Kwa upande mwingine, Mhandisi Mgaya amesema chuo kitaendelea kusimamia na kuboresha utoaji wa mafunzo, ufanyaji wa tafiti na utoaji wa ushauri wa Kitaalam ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata ujuzi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa.
Aidha, NIT itaendelea kubeba dhamana ya kuzalisha nguvu kazi mahiri na kujenga uwezo wa kiteknolojia katika sekta ya usafirishaji ili kuwa na uhakika wa uzalishaji wenye tija kwenye uchumi wa kimaendeleo. Ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Taifa linazalisha rasilimali watu yenye ubora wa kujiajiri na kuajiriwa katika soko la kimataifa.