Na Georgina Misama, Maelezo
Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inatarajia kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa uwekezaji katika eneo la Kurasini lenye ukubwa wa hekari sita lililopo wilayani Temeke Jijini Dar es salaam litakalojulikana kama Mtaa wa Viwanda na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (Kurasini Industrial Park and Business Centre)
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya eneo hilo, Waziri wa Viwanda na Biashar,a Prof. Kitila Mkumbo alisema kuwa katika mwaka huu wa fedha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo ambayo yanatarajiwa kukamilika Februari, 2022.
Prof. Kitila alifafanua kuwa mradi huo utahusisha mambo makubwa matano ambayo ni ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, ujenzi wa viwanda vya kutengeneza na kuunganisha bidhaa mbalimbali ikiwemo bidhaa za umeme, ujenzi wa kituo cha kimataifa cha mazao ya kilimo na biashara, ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mbogamboga katika hali ya uasili wa baridi na ujenzi wa kituo cha pamoja cha kutoa huduma za kijamii (One Stop Service Centre).
“Kwa sababu hiki ni Kituo cha Kimataifa cha Biashara, kutakuwa na huduma zote kama vile utoaji wa viza, hati ya kusafiria, Vibali vya kusafirisha bidhaa nje ya nchi hivyo ninaomba ushirikikano wa wadau wote muhimu katika kufanikisha mradi huu muhimu kwa uchumi wan chi yetu,” alisema Prof. Kitila.
Prof. Kitila aliongeza kuwa mradu huu utatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali kupitia (EPZA) na wawekezaji kutoka sekta binafsi ambapo tayari mchakato wa kuwabainisha umekamilika na makampuni matano yamebainishwa ambayo ni DP World (Dubai, UAE), Elsewedy (Egypt), Agility (Dubai, UAE),Galco (Tanzania) na Shanghai Lingang Group Co. Ltd. (China) hatua inayofuata ni kufanyiwa tathmini na uchambuzi wa kina ili kumpata mwekezaji atakaeshirikiana na Serikali katika kutekeleza mradi huo unaotarajiwa kuanza Juni, 2022.
Aidha, Prof. Kilita ameeleza kuwa, kazi kubwa ya Serikali ni kutengeneza mazingira wezeshi ikiwemo ujenzi wa barabara, miundombinu ya maji, umeme na ujenzi wa ukuta kuzunguka eneo hilo kazi ambayo inatarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni.
Mradi huu ni moja ya miradi mikubwa michache barani Afrika ambayo chimbuko lake ni mwaka 2009 ambapo unatekelezwa katika nchi nne za Afrika, Tanzania ikiwa moja wapo. Kukamilika kwa mradi kutato fursa kwa wafanyabishara wa ndani na nje ya nchi kuuza na kunua bidhaa katika kituo hicho.