Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa, kwa sasa Serikali inakamilisha kazi ya uandaaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2033.
Amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Jacqueline Ngonyani Msongozi (Viti Maalum) aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kuweka ruzuku kwenye nishati ya gesi ili wananchi waweze kumudu kununua.
Akijibu swali hilo, Mhe. Kapinga amesema “Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kutatua vikwazo vinavyokwamisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza gharama za upatikanaji wa nishati safi, vifaa na majiko sanifu ya kupikia.”
Ameeleza kuwa, Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia ni Ajenda ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na hilo lilitiliwa mkazo katika Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) Dubai, ambapo Rais, Dkt. Samia alizindua mkakati wa nishati safi ya kupikia kwa wanawake Afrika hivyo Wizara ya Nishati inalibeba suala la nishati safi ya kupikia kwa uzito mkubwa.
Kuhusu ruzuku kwa mitungi ya gesi ili kupunguza gharama ya mitungi hiyo, Naibu Waziri amesema kuwa, tayari kuna programu na miradi mbalimbali inayoendelea akitolea mfano programu ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya (EU) ambapo Mawakala wanawezeshwa kifedha ili kupunguza bei ya mitungi ya gesi kwa watu wanaonunua mitungi hiyo kwa mara ya kwanza na kwamba Serikali itaendelea kubuni miradi na kutafuta fedha ili wananchi wapate gesi kwa gharama nafuu.
Ameongeza kuwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikibuni na kutekeleza sera na mikakati yenye lengo za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na utunzaji wa mazingira.
Vilevile, Mhe. Kapinga amesema kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza mradi wa kusambaza nishati safi ya kupikia kwenye taasisi mbalimbali ikiwemo magereza, kambi za jeshi, shule za msingi na Sekondari na kwamba zoezi hili ni endelevu kwani Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuzifikia taasisi nyingi zaidi.
Mhe. Kapinga amesema kuwa, jitihada hizo zinazofanywa na Serikali ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 inayoielekeza Serikali kuchukua hatua madhubuti za kufanikisha matumizi ya nishati na vifaa sahihi vya kupikia.