Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Ina Mpango wa Kuwanoa Makocha wa Ndani - Mhe. Gekul
Jun 22, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul akizungumza Bungeni leo jijini Dodoma

Na Shamimu Nyaki - WUSM, Dodoma

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amesema Serikali inawajali Makocha wazawa ambao wana sifa pia kupitia Mpango Mkakati wa kuendeleza Michezo wa Mwaka 2021 hadi 2031 imeweka kozi na mafunzo mbalimbali kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi Makocha hao.

Mhe. Gekul  amesema hayo leo Juni 22, 2022  Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu  swali la Mhe. Antipas Zeno (Malinyi) aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali wa kulinda Ajira za Makocha Wazawa na kuwaongezea ujuzi wa kufundisha nje ya nchi.

"Serikali inajali ajira za wazawa na kwa sasa Kozi fupi mbalimbali zinatolewa kupitia Chuo Cha Michezo Malya na Butimba  ambapo hadi sasa   Vijana 20 wanapatiwa mafunzo hayo na watakapofuzu watapewa fursa", amesema Mhe. Gekul.

Mhe. Gekul ameongeza kuwa Tanzania ina Makocha 19 ambao wana viwango wa CAF "A" Diploma ambao wanakidhi viwango kufundisha nje ya nchi.

Akiendelea kujibu maswali ya Wabunge waliouliza  kuhusu mpango wa kuendeleza Makocha Wanawake akiwemo Mhe. Fatma Taufiq,   Mhe. Gekul amesema kwamba Makocha Wanawake  wenye sifa wanapewa kipaumbele na wanahamaishwa kujiendeleza kupata Kozi mbalimbali zinazotolewa ili waongeze sifa na kupata madaraja ya juu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Gekul amesema kuwa, suala la Makocha waliofuzu Kozi na Mafunzo yaliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF)  Mwaka 2016 ambao mpaka leo hawajapatiwa vyeti vyao, Amesema kwamba suala hilo linashughulikiwa na litakapokamilika Makocha hao watapatiwa vyeti Vyao.

Aidha, katika swali lililoulizwa na Mhe. Mohamed Said Issa (Konde) kuhusu Zanzibar Football Federation (ZFA) kupitia TFF kupata faida zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Mhe. Gekul amesema suala hilo linashughulikiwa na hivi karibuni Mawaziri wanaosimama Michezo Tanzania Bara na Zanzibar watakaa kikao ambacho pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha Zanzibar inafaidika na mgao wa FIFA.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi