Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Senyamule Asisitiza Matumizi ya Matokeo ya Sensa kwa Madiwani, Watendaji
Dec 11, 2022

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule leo tarehe 11/12/2022 amefungua mafunzo ya Madiwani na Watendaji wa Kata na Mitaa ya Jiji la Dodoma. Mafunzo hayo yanahusu matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa ajili ya mipango jumuishi na maendeleo endelevu ya Jiji la Dodoma.

Akifungua mafunzo hayo katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Mhe. Senyamule amesema katika kutatua changamoto ya upatikanaji wa takwimu na kupunguza gharama za kufanya Sensa tatu tofauti, Serikali iliamua kufanya Sensa zote tatu kwa pamoja chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 ilifanyika kwa pamoja na mazoezi mengine makuu mawili; Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi. Kwa kipindi kirefu nchi yetu ilikuwa haina takwimu za majengo za kutosha na za uhakika ambazo zimeunganishwa na takwimu za watu, hali zao za makazi na anwani za makazi kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo ya sekta ya nyumba” alisisitiza Mhe. Senyamule.

Amesema matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi yanakwenda kubadilisha sura na mwenendo wa utungaji sera, upangaji wa mipango, tathmini ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuimarisha ustawi wa wananchi na kuwahimiza Madiwani na Watendaji wa Kata na Mitaa kutumia mafunzo hayo kama nyenzo muhimu ya kutafsiri kwa vitendo matokeo ya Sensa katika maeneo yao.

“Kwetu sisi hapa Dodoma tuna kazi kubwa sana ya kuendelea na kazi ya kuupanga huu mji ipasavyo. Matokeo yameonesha kuwa idadi ya watu imeendelea kuongezeka kutoka watu milioni 2.1 mwaka 2012 hadi watu milioni 3.1 mwaka 2022 sawa na kasi ya ongezeko la asilimia 3.9 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita” alisisitiza Mhe. Senyamule.

Amewaagiza Wadiwani na Watendaji wa Kata na Mitaa ya Jiji la Dodoma kukaa na Wakurugenzi wa Halmashauri zao na kufanyia kazi kwa kina matokeo ya sensa tatu na kusisitiza kupata mrejesho wa haraka kujua yatakayobainika kuhusu huduma za jamii zilizopo, majengo na anwani za makazi.

“Nitumie nafasi hii kuwaagiza Wakuu wote wa Wilaya mliopo kuwa Serikali imetumia raslimali fedha za kukusanya taarifa hizi na sisi tumebahatika kupata mafunzo haya kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Hivyo, napenda kuwaelekeza mnipatie mrejesho wa wapi tunatakiwa kuboresha zaidi na hususan katika sekta za jamii kama vile Shule za Msingi na Sekondari”, Mhe. Senyamule aliagiza.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa amesema wameanza mafunzo haya kwa Watendaji wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwa yataainisha viashiria vya kiuchumi, kimaendeleo na kijamii kwa ajili ya mipango jumuishi.

Naye Kamisaa wa Sensa Spika mstaafu, Mhe. Anne Makinda amesema zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 imelenga kuhakikisha takwimu si za kupita bali ziishi kwa miaka 10. 

Mkoa wa Dodoma umekuwa ni Mkoa wa kwanza kupatiwa mafunzo na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuhusu matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 yanayoongozwa na kaulimbiu isemayo: “Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa Mipango Jumuishi na Maendeleo Endelevu”.

Serikali imeandaa Mwongozo Maalumu wa Kitaifa wa Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa lengo la kuongeza uelewa, uwazi na kupanua wigo wa matumizi ya matokeo hayo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuweka mipango jumuishi kwa maendeleo endelevu ya kijamii, kiuchumi na mazingira.

Mipangilio
Marekebisho ya Lugha
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi