Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Sekta za Afya, Elimu, Maji, Utalii, Michezo Zaguswa Tamasha la Kizimkazi
Aug 31, 2023
Sekta za Afya, Elimu, Maji, Utalii, Michezo Zaguswa Tamasha la Kizimkazi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa pamoja na viongozi mbalimbali wakati akipokea Maandamano ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) (hayapo pichani) mara baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Paje kwa ajili ya kilele cha Tamasha la Kizimkazi lililofanyika Zanzibar tarehe 31 Agosti, 2023.
Na Mwandishi Wetu - MAELEZO

Tamasha la Kizimkazi ambalo leo limefikia kilele chake katika Viwanja vya Kashangae katika Kata ya Paje wilayani Kusini Unguja na kugusa Sekta za Afya, Elimu, Maji na Michezo kupitia miradi mbalimbali iliyozinduliwa na mingine kuwekwa mawe ya msingi katika wiki la tamasha hilo.

Tamasha hilo ambalo kwa mwaka huu limefanyika kwa mara ya Saba wilayani humo likiwa na lengo kujitathmini na kujipanga kimkakati kwa ajili ya maendeleo ya wilaya hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni muasisi wa tamasha hilo, amesema, ”katika tamasha la mwaka huu tumeweka mawe ya msingi na kuzindua miradi kadhaa ikiwemo Sekta ya Elimu, Afya, Elimu, Maji, Utalii na Michezo”.

Amesema kuwa, katika Sekta ya Elimu TASAF wamefanyia ukarabati moja ya Shule Kongwe ya Kizimkazi, ambayo ina zaidi ya miaka mia, iliyojengwa mwaka 1910.

Vilevile TASAF imekarabati ukumbi wa mitihani kwa ajili ya wanafunzi wa Shuke ya Sekondari ya Kizimkazi.

“Tumefungua madarasa 11 ambayo yamefanyiwa marekebisho na TASAF ndani ya shule ya Kizimkazi. Katika Kijiji cha Muyuni, madarasa Sita yamefanyiwa ukarabati mkubwa na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ). Pia kumejengwa ukumbi wa mitihani Shule ya Msingi Muyuni ambao ni mchango wa Benki ya Azania,” amesema Mhe. Rais.

Viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wakiwa kwenye viwanja vya Paje kwa ajili ya kuhudhuria Kilele cha Tamasha la Kizimkazi lililofanyika Zanzibar tarehe 31 Agosti, 2023.

Kwa upande wa Sekta ya Afya Mhe. Rais amesema, “tumezindua Kituo cha Afya kipya kilichojengwa na wafadhili kutoka Oman, kilichopo Dimbani, ambapo pia Vodacom wameweka mfumo wa M-MAMA katika kituo hiko cha Mama na Mtoto. Kituo hicho pia kimepatiwa gari”.

Vilevile kumewekwa jiwe la msingi la hospitali maalum ya Wananchi wa Mkunguni ambayo kwa sehemu itadhaminiwa na NBC na wafadhili wengine wanaoendelea kujitokeza.

Sambasamba na hayo, pia  Kizimkazi kuna ujenzi wa Soko ambalo linafadhiliwa na Benki ya CRDB.

“Tumezindua mradi wa maji ambao kwa miaka kadhaa kijiji chetu cha Kizimkazi kulikuwa na matatizo ya maji. DAWASA wameleta utaalam, hivyo tumeweza kuondoa tatizo la maji,” amesema Mhe. Rais.

Aidha kwa upande wa Utalii, imezinduliwa hoteli ya nyota tano ya Kwanza Hoteli, ambayo imetoa ajira kwa watu 300 wa ndani na nje ya Kijiji cha Kizimkazi pamoja na Tanzania Bara.

Pia kumezinduliwa matawi ya benki ya NMB na PBZ katika Kata ya Paje, ambazo tayari zimeanza kazi na kupata wateja.

“Tumeweka jiwe la msingi kiwanja cha kuchezea watoto Kizimkazi, ambaye mfadhili wake ni Camel Oil, ambacho kitachukua watoto 400, na  kitakuwa na mambo yote ya kufurahisha watoto,” amefafanua Mhe. Rais.

Tamasha la mwaka huu limebeba kauli mbiu inayosema, “Tuwalinde Kimaadili Watoto Wetu kwa Maslahi ya Taifa”.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi