Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Sekta ya Madini Nguzo Muhimu Maendeleo ya Nchi
Oct 25, 2023
Sekta ya Madini Nguzo Muhimu Maendeleo ya Nchi
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023 jijini Dar es salaam.
Na Mwandishi Wetu

Imeelezwa kuwa, Sekta ya Madini ni nguzo muhimu na chachu ya maendeleo ya uchumi wa nchi kupitia rasilimali madini iliyopo nchini.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 25, 2023 na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Jukwaa la Madini na Uwekezaji  Tanzania 2023 jijini Dar es salaam.

"Kutokana na umuhimu wa Sekta ya Madini katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi," amesema Dkt. Biteko

Amesema, Sekta ya Madini inafungamanishwa na sekta nyingine za kiuchumi kama vile viwanda na kilimo ili kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotumia madini kama malighafi mfano mbolea, betri za magari, simu, kompyuta na bidhaa nyingine.

"Niwahakikishie kuwa, mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Madini yameendelea kuboreshwa na kuwa rafiki zaidi. Nafurahi kusema kuwa, hadi sasa jumla ya kampuni tisa za kimataifa za uchimbaji mkubwa wa madini zimeingia ubia na Serikali katika uchimbaji wa madini mbalimbali ikiwemo madini ya nikeli, kinywe, heavy mineral sands (mchanga bahari), Rare Earth Elements, dhahabu na almasi," ameongeza Dkt. Biteko.

Aidha, Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa miundombinu mbalimbali inaboreshwa ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa ili kuhakikisha nchi ya Tanzania inanufaika na rasilimali madini, wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za Sekta ya Madini ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi na Serikali inapata mapato stahiki.

"Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za Sekta ya Madini ili kuhakikisha kuwa mchango wake unakua hadi kufikia asilimia 10 ya Pato la Taifa kufikia  mwaka 2025 kama ilivyo katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025. Tutashirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta kuhakisha lengo hilo linafikiwa," ameongeza Waziri Mavunde.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi