Asilimia 69 ya Ardhi inafikiwa na Mawasiliano ya Simu za Kiganjani
Na. Georgina Misama – MAELEZO, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Sekta ya Habari na Mawasiliano nchini imekua kwa kasi ya asilimia 8.4 kwa mwaka 2020 ambapo kumekuwa na ongezeko la upatikanaji na matumizi ya huduma za mawasiliano na kusambaa kwa huduma zitolewazo na Vyombo vya Habari.
Katika hotuba yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2022/2023 aliyoitoa leo Mei 20, 2022 Bungeni Dodoma, Waziri Nape amesema kulingana na uchambuzi uliofanywa na Wizara husika mwaka 2021 unaonyesha kwamba hivi sasa asilimia 69 ya ardhi ya Tanzania inafikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu za kiganjani ambapo kumekuwa na ongezeko la usajili wa laini za simu, watumiaji wa intaneti na watumiaji wa huduma ya kutuma na kupokea fedha.
“ Takwimu zinaonyesha kuwa laini za simu zilizosajiliwa kutoka mwezi Aprili 2021 zimeongezeka kwa asilimia 4.5, watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka milioni 29.1 Aprili, 2021 hadi kufikia milioni 29.9 Aprili 2022 sawa na ongezeko la asilimia 2.7, lakini pia watumiaji wa huduma za kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu wameongezeka kwa asilimia 30.8,” alisema Waziri Nape.
Aidha, Waziri Nape amesema kuwa pamoja na kuwepo kwa eneo kubwa lenye mawasiliano ya intaneti ni asilimia 27 tu ya watumiaji wa vifaa vya mawasiliano wanatumia intaneti hiyo pamoja na jitihada za Serikali kuondoa kodi kwenye vifaa vya mawasiliano kama vile laptop, tablet, kumeongeza idadi ya simu janja kwa asilimia mbili (2) tu.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Anne Kilango Malechela alisema kuwa uwezeshaji kwenye Sekta ya Mawasiliano ni chachu kubwa ya maendeleo ya uchumi, na kuongeza kuwa ni muhimu Serikali kuhakikisha Sekta hii inastawi na kuchangia kwa kiwango kikubwa zaidi katika maendeleo ya nchi na uchumi.