Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Rwanda zimeendelea kunufaika kiuchumi kupitia ushirikiano wa karibu katika biashara na uwekezaji, huku miradi 142 iliyosajiliwa ikitoa ajira kwa Watanzania 2,225.

Rais Samia ameyasema hayo leo Mei 3, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kufanya mazungumzo na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Paul Kagame, aliyewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Amesema nchi hizo mbili zimekubaliana kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri na huduma za usafirishaji ili kurahisisha biashara na kuongeza fursa za uwekezaji.

“Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 70 ya mizigo ya Rwanda inapitia bandari za Tanzania, hivyo ni jukumu letu kuhakikisha huduma zinakuwa bora na za uhakika,” amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Rwanda kimefikia shilingi bilioni 644 mwaka 2025, hali inayoakisi ukuaji wa mahusiano ya kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wa uwekezaji, Rais Samia amesema kuwa kuanzia Machi 1997 hadi Machi 2026, miradi 142 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 325.5 imesajiliwa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza uchumi na ajira kwa wananchi.