Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Samia Awaasa Waumini Kuhusu Kujitoa kwa Mwenyezi Mungu
Feb 26, 2025
Samia Awaasa Waumini Kuhusu Kujitoa kwa Mwenyezi Mungu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza viongozi mbalimbali pamoja na Waumini wa dini ya Kiislam mara baada ya kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa uliopo Tanga mjini tarehe 26 Februari, 2025.
Na Grace Semfuko-MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kujitoa kwa hali na mali kwa ajili ya kusaidia miradi ya maendeleo na shughuli za kijamii ni muhimu, na ni baraka kwa Mwenyezi Mungu, hivyo jamii na watu wenye uwezo na wenye maeneo makubwa ambayo hawayaendelezi wafukirie kuyatoa ili yaweze kuwanufaisha wengi zaidi.

Rais Samia amesema hayo leo Februari 26, 2025 mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi la upanuzi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa uliopo Tanga Mjini, ambapo eneo ulipojengwa msikiti huo lilitolewa wakfu na Sharrif Mohamed Haidar.

"Mzee wetu huyu aliishi kwa vitendo, ndugu zangu sote tunatambua thamani tuliyoipa ardhi, watu wanapigana, wanauana kwa sababu ya ardhi, ndugu wanagombana kisa ardhi, majirani hawasemeshani kisa wameingiliana kwenye ardhi, mataifa yanaingia vitani kwa sababu ya ardhi, lakini mzee wetu huyu aliona atoe wakfu sehemu ya ardhi yake aliyoimiliki kwa maslahi ya vizazi vijavyo. Hili ni jambo kubwa sana " ameeleza Rais Samia.

Amesema ili kutambua ukubwa wa jambo alilofanya mzee huyo, jamii inapaswa kujiuliza ni wangapi wanawaza kuvisaidia vizazi vya kesho, na kuongeza kuwa watu wengi hawajaweza kuzingatia vizazi vya kesho na ndugu zao.

"Mzee wetu huyu akiongozwa na imani yake, aliamua kutoa sehemu ya ardhi yake, tena katika mji wa watu waungwana kama hili Jiji la Tanga ambako ardhi ina thamani kubwa na inapanda thamani kila uchao, wakfu huo unatufundisha somo kubwa na muhimu sana" amesisitiza.

Amesema jamii inapaswa kujiuliza ni kwa vipi wanakwamisha miradi mikubwa ya maendeleo tena inayowanufaisha mpaka wao wenyewe kwa kumiliki maeneo makubwa ambayo hawayaendelezi.

"Leo hii tujiulize ni wangapi wanaokwamisha miradi mikubwa ya maendeleo, tena ni miradi inayonufaisha hata wao wenyewe, basi kwa uchoyo tu wa nafsi zetu, Ni wangapi wanashikilia maeneo makubwa ya ardhi ambayo hawayaendelezi, lakini hawayaachii kwa walio tayari kuyaendeleza, kwa hiyo kitu alichofanya Mzee wetu Almahruoum Shariff Haidery Bin Ahmed ni jambo kubwa sana" amesema Rais Samia.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi