Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Sakata la Makinikia: Watanzania Tuondoe Hofu, Tumuamini Rais Wetu.
Jun 20, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu,MAELEZO.

Tangu uongozi wa Kampuni ya Barrick, ambayo ndio yenye hisa nyingi katika kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia iliyo katika mgogoro na Serikali kutangaza kuwa ipo tayari kutafuta mwafaka kwa njia ya mazungumzo, kumekuwepo na baadhi ya watanzania wanaonesha wasiwasi juu ya kufanikiwa kwa jambo hilo. Katika Makala hii Mwandishi Said Ameir wa Idara- Habari MAELEZO anasisitiza kuwa watanzania hawapaswi kuwa na wasi wasi hata chembe.

Ni tangazo lililoleta faraja kwa watanzania wengi kwa kuwa wanaamimi kuwa hatua ya kufanya mazungumzo na ile kauli ya Mwenyekiti wa Barrick Profesa John Thornton kuwa wapo tayari kuilipa Tanzania kila kile kilichostahili ambacho kampuni ya Acacia haikuilipa, ni uamuzi mwafaka.

Kwanza imani ya watanzania wengi imejengwa kutokana na uthabiti wa matokeo ya Kamati zote mbili; Kamati ya Kuchunguza Aina na Viwango vya Madini Vilivyomo Katika Mchanga wa Madini Unaosafirishwa Nje na Kamati ya Kuchunguza Masuala ya Kisheria na Kiuchumi ya Mchanga huo.

Pili, wamejenga imani zaidi kwa kuangalia hatua ya kampuni ya Barrick ya kumtuma kiongozi wao wa juu kuja Tanzania na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli, ambaye ndie aliyeunda Kamati mbili kuchunguza kadhia.

Zaidi watanzania, wanaitafsiri kauli ya Profesa Thornton ya kuwa kampuni yake iko tayari kuilipa Tanzania fedha zote ambazo ilistahili kulipwa na Acacia kuwa ni kauli yeye kuthibitisha ukweli wa madai ya serikali kuwa nchi yao imekuwa ikiibiwa na Acacia.

Kwa hivyo, hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi wa kupata haki, sio tu kupitia mazungumzo hayo bali hata ikilazimu kupitia vyombo vya sheria vya kimataifa.

Hata hivyo wako baadhi kupitia mitandao ya kijamii na katika baadhi ya magazeti wamekuwa wakijaribu kuonesha kama kwamba jambo hilo Rais na Serikali ‘wamebugi step’ wakimaanisha kama vile hiyo ni janja ya mwekezaji tu na kwamba fedha hizo hazitalipwa.

Baadhi wamekuwa wakitumia mbinu za kuonesha uzito wa majadilinao hayo kwa kulinganisha wasifu na umaarufu wa wajumbe wa bodi wa makampuni ya Barrick na Acacia huku wakihoji ni akina nani Tanzania wanaweza kupambana na wajumbe hao.

Aidha watu hao wanakoleza hoja yao hiyo kwa kunukuu nadharia za taaluma ya mazungumzo kutaka kuonesha kuwa watanzania wako katika nafasi finyu kufanikiwa katika mazungumzo hayo.

Ni nyema hapa kuweka sawa mambo mawili matatu ili jambo hili lieleweke vizuri kwa faida ya watanzania wote. Kitu muhimu ni kupambanua kuwa mazungumzo ya Tanzania na Acacia/Barrick yatakuwa katika maeneo mawili makuu.

Kwanza ni kuhusu utekelelezaji wa mkataba uliopo kati ya Serikali na Acacia ambapo matokeo ya Kamati zote mbili yanaonesha kuwa mkataba haukutelekezwa ipasavyo kutokana na udanganyifu mkubwa uliofanywa ili kukwepa kodi na stahiki nyingine ambazo Tanzania ilipaswa kulipwa.

Udanganyifu huo ulifanyika kwa kampuni ya Acacia kutoa taarifa zisizo sahihi; kwa mfano kutoeleza madini zaidi yaliyomo katika mchanga na kutolipa mirahaba ya madini hayo. Vitu kama hivyo havina mjadala bali ni kazi ya kuthibitisha tu. Na hapa lazima kueleza kuwa mzigo mzito uko kwa Acacia kuzipinga hoja za Kamati za Rais hadi kujisafisha.

Pili ni suala la mkataba uliopo ambao uongozi wa Awamu ya Tano pamoja na watanzania wote wanauona hauna maslahi kwa Taifa. Umewalalia mno! Hapa ndio kwenye mazungumzo ambayo inaweza kuelezwa kuwa hayatakuwa ya mteremko.

Turudi kuangalia suala la bodi hizi kuwa na majina ya watu wakubwa na mashuhuri. Hili si jambo jipya wala la kushangaza. Huu ndio utamaduni wa dunia nzima ya biashara za kinyonyaji. Tunaweza kujiuliza ni kampuni gani kubwa za nje humu nchini hazina Wenyeviti wa Bodi au Wajumbe wa Bodi ambao si watu wenye ushawishi na wanaojulikana kwa namna moja ua nyingine katika ngazi ya uongozi wa Serikali.

Je, shabaha yao ni nini? Kwa ukweli, shabaha kubwa ya kuwekwa watu hao katika Bodi ni kutaka kupata fursa za kuingia katika ofisi za Serikali na kusukuma mambo yao yasikwame ikiwemo huo ukwepaji kodi. Ni suala ya PR tu.

Lakini si dhani kuma watu hao ndio wanaofanya mazungumzo, bali wataalamu wao kama ambavyo Tanzania itapeleka watalamu wake. Tanzania ina wataalamu waliobobea katika masuala yote ambayo yatazungumziwa katika mazungumzo hayo.

Ikumbukwe kuwa Tanzania inakwenda katika mazungumzo hayo ya ajenda zake mbili kuu. Kulipwa stahiki zake ilizokoseshwa kutokana na udanganyifu wa kampuni ya Acacia kama zilivyoeleza Kamati za Rais na pia kutaka mkataba wenye maslahi kwa pande zote kitu ambacho hata Profesa Thornton alionesha nia ya kukikubali.

Hapana shaka yeyote kuwa Barrick hawatafanya makosa ya kung’ang’ania kuendelea na mikataba kandamizi kama iliyopo sasa kwa sababu mazingira hayaruhusu tena. Ni vizuri watu wakaliangalia suala hili kwa mapana zaidi na athari zake kwa Barrick na Acacia.

Ilielezwa kuwa mgogoro unaofanana na huu ulitokea kati ya Barrick na nchi za Saudi Arabia na visiwa vya Dominica vilivyoko katika visiwa vya Caribbean, ambapo serikali ya nchi hiyo ilizuia shehena nzima ya dhahabu yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 20 isisafirishwe.

Hata hivyo tukio hilo la Dominca ingawa linashabihiana lakini haliwezi kulinganishwa na suala la Tanzania kwa kuwa Tanzania yenyewe imekwenda mbali zaidi kwa kufanya utafiti kuthibitisha wasiwasi iliokuwa nao kuwa haitendewi haki na kampuni ya Acacia.

Mazungumzo kati ya Barrick na Tanzania yanatarajiwa kuwa ya aina yake na kufuatiliwa kwa karibu   na vyombo vya habari humu nchini na nje pamoja na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu na unyonyaji dhidi ya nchi masikini hasa ikizingatiwa umaarufu wa Rais Magufuli kote duniani hivi sasa.

Dunia itataka kujua nguvu na harakati za Rais Magufuli za kutetea maslahi ya watu wake na bila ya shaka ye yote Rais Magufuli na watanzania wanataka kuhakikisha kuwa haki inatendeka na watanzania wanafaidika na rasilimali zake.

Kwa hivyo hata kama Barrick italeta wabobezi wa mazungumzo, Tanzania pia inao wataalamu waliobobea katika sekta hiyo ambao wametaalamika katika masuala ya sekta ya madini katika njanja za tekinolojia, sheria, mikataba, kodi na miraha nk.

Watanzania hawana haja ya kuogopa majina wa wenyekiti au wajumbe wa Bodi ya Barrick na Acacia. Kama ilivyoelezwa hapo awali hao si wataalamu bali ni watu kujenga mahusiano na kurahisha mambo ya makampuni yao yaende bila vikwazo ikiwemo hili la mikataba mibovu kama hii!

Majina yao na nyadhifa zao wakati mwingine zinawapa faida ya kutokuulizwa na kupewa upendeleo kwa kampuni hizo lakini si utalaamu. Ni sehemu tu ya kuendeleza unafiki wa nchi za tajiri katika kuzinyonya nchi masikini.

Kitu muhimu sasa watanzania ni kusubiri timu ya mazungumzo itajwe na kuipa kila aina ya ushirikiano ili ipate nguvu na ione fahari kuwawakilisha watanzania wenzao katika kutetea haki na maslahi ya watanzania.

Katika hali kama iliyoko sasa hayumkini hata kidogo kwa baadhi ya watanzania, iwe mitaani, mitandaoni au kupitia vyombo vya habari kuanza kuanzisha hadithi za kuwatia wasiwasi na kuwakatisha tamaa wananchi ambao wamejenga imani kubwa kwa Rais wao na serikali yake.

Jitihada za Rais kutetea rasilimali za nchi zimeamsha hamasa na hisia za wananchi kuipenda nchi yao na kuonesha uzalando wao, zimejenga matumaini makubwa kwa wananchi na zimejengea ari na moyo wa kupigania maslahi ya nchi yao. Ni wakati watanzania kuungana katika vita hii ya kutetea rasilimali kwa maslahi na maendelo ya nchi yao.

MWISHO

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi