Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Safari za Treni Kurejea Ndani ya Saa 24 – Prof. Mbarawa
Mar 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Serikali imesema ujenzi wa daraja jipya la reli ya kati  linalojengwa  baada ya daraja la zamani kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika eneo la kidete wilayani Kilosa litakamilika ndani ya saa 24 ili kuruhusu huduma ya treni kuendelea.

Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kurejeshwa kwa safari za treni kutapunguza changamoto ya usafirishaji wa abiria na mizigo hususani kwa mikoa ya pembezoni mwa Tanzania.

“Leo ni takribani siku ya kumi hakuna bidhaa zinazokwenda mikoa ya pembezoni mwa Tanzania kama Kigoma sababu wanategemea sana reli hii hasa wafanyabiashara, mtakampokamilisha ujenzi huu kutawapunguzia adha wananchi wa maeneo hayo”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa amelipongeza Shirika la Reli Tanzania (TRC), kwa kufanya maamuzi ya haraka na kuhakikisha huduma zinarejea ndani ya muda mfupi na kuwataka kuzingatia thamani ya fedha kwa fedha zote zinazotumika nyakati za dharura.

Muonekano wa daraja la reli lililosombwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini katika stesheni ya Kidete, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro. Kusombwa kwa daraja hilo kumesimamisha huduma za treni kwa takribani siku 10.

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa ameupongeza Uongozi wa Yapi Markezi kwa kushirikiana kwa karibu na TRC katika kutekeleza ujenzi wa daraja hilo kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vilivyokubalika.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Shirika linafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha huduma za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo zinarejea.

Masanja ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo umegharimu kiasi cha shilngi takribani bilioni 3 na linatarajiwa kukamilika muda wowote kuanzia sasa na hatimaye kuruhusu treni ya majaribio kupita.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Makame Mbarawa ameitaka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuangalia upya vipengele vya ujenzi wa mradi wa Kiwanda cha Mkulazi ili kujiridhisha na vipengele vilivyopo kama vina tija na vimezingatia uhalisia.

Prof. Mbarawa ameeleza umuhimu wa kukamilisha mradi huo na kueleza kuwa Serikali haitosita kuvunja mkataba na Mkandarasi Kampuni ya Kay Bouvet Enginerring Ltd ya nchini India itakapoona hairidhishwi na maendeleo ya mradi huo.

“Hatuwezi kukubali mwende namna hii, mmeshaandikiwa barua za onyo mbili ikiandikwa ya tatu mkataba utakuwa umeishia hapo, sababu hamjatilia uzito na kasi yenu haioneshi kama mtamaliza kwa wakati”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Kampuni ya Mkulazi, Selestine Some  amesema mradi huo unapaswa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu na kazi zinazoendelea zimefikia asimlia zaidi ya 30.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi